MADA: Dhana ya Maadili Katika Jamii za Asili ya Kitanzania
Maadili katika jamii za asili za Kitanzania ni sehemu muhimu ya utamaduni wa makabila mbalimbali nchini Tanzania. Dhana hii inahusu kanuni na miongozo ya kimaadili ambayo inaongoza maisha na mahusiano ya watu katika jamii hizo. Maadili ya jamii hizi pia yalijikita kwenye mila na desturi za jamii inayohusika.
Katika jamii za Kitanzania kuna makundi mbalimbali, hivyo maadili yanaweza kuwa ya jamii nzima ama ya kundi fulani katika jamii hiyo. Maadili ni muhimu kwa kuwa yanawawezesha wanajamii kuishi kwa kufuata mienendo iliyokubalika na hivyo kupunguza migongano katika jamii.
Hata katika jamii za Wabantu, Wakushito, Wakichembe na Wanilo kulikuwa na mila na desturi zilizolenga kukuza maadili katika nyanja mbalimbali za maisha yao. Mila na desturi za jamii hizo zilitofautiana kutokana na kuwapo kwa mifumo tofauti ya kiuchumi, kijamii, kiutawala na kimazingira. Hata hivyo, kwa ujumla ujenzi wa maadili katika jamii hizo ulikuwa na malengo yafuatayo:
Maadili katika jamii za asili za Kitanzania mara nyingi yanahimiza ushirikiano na umoja. Watu wanafundishwa kushirikiana na kusaidiana katika kazi za kilimo, ufugaji, na shughuli nyingine za kijamii. Familia na jamii nzima zinaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika maisha ya mtu binafsi.
Lengo hili lililenga kujenga jamii yenye amani, umoja, na maendeleo endelevu.
Heshima kwa wazee na viongozi wa kijadi ni sehemu muhimu ya maadili. Wazee huchukuliwa kama chanzo cha hekima na uongozi katika jamii na wanaheshimiwa kwa kina.
Hii ililenga kuhamasisha jamii kwa kuelimisha umuhimu wa kazi na mchango wake katika kujenga maisha bora. Hii inaweza kufanyika kupitia mafunzo, semina, na mikutano ya kijamii.
Maadili katika lengo hili yalisisitiza kuheshima kwa mazingira na asili. Watu wanafundishwa kuitunza ardhi, maji, na rasilimali za asili kwa kizazi kijacho. Uvutano wa desturi za kidini na za kishirikiana na mazingira ni sehemu muhimu ya maadili.
Jamil za asili za Kitanzania zina utajiri wa mila, tamaduni na desturi. Kuheshimu na kusimamia utamaduni na mila za kabila ni sehemu muhimu ya maadili. Kwa mfano, sherehe za kimila na mila za ndoa zinachukuliwa kwa umuhimu mkubwa.
Ukarimu ni sehemu muhimu ya maadili. Watu wanafundishwa kutoa makazi na chakula kwa wageni na kusaidiana katika nyakati za shida. Kusaidiana na kusimama pamoja ni kanuni kuu.
Kwa ujumla, maadili haya yalichangia kudumisha utamaduni na utambulisho wa jamii za asili za Kitanzania na kuimarisha mahusiano ya kijamii katika jamii hizo.
Maadili ya Asili ya Jamii za Kitanzania Katika Nyanja za Kiutamaduni
Kwa ujumla, maadili katika jamii za Kitanzania kiutamaduni yanahusisha uaminifu, heshima kwa wazee na familia, ukarimu, kuheshimu utamaduni na mila na uadilifu. Aidha, dhima za mila na desturi za jamii za Wabantu, Wakushito, Wakichembe na Wanilo zililenga kukuza maadili katika nyanja za heshima, ndoa, tabia njema, chakula, imani, milko, malezi na makuzi na taratibu za maisha zilizotumika katika jamii hizo. Maadili haya ni muhimu hata katika nyakati za sasa ili kudumisha mahusiano ya familia na kulea vizazi vijavyo kwa mujibu wa tamaduni na mila za Kitanzania.
Ufuatao ni ufafanuzi wa maadili ya asili ya jamii za Kitanzania katika eneo la kiutamaduni:
- Uaminifu katika ndoa: Katika ndoa, uaminifu wa mke na mume ulikuwa ni kama sehemu ya maadili. Ndoa ilichukuliwa kuwa sakramenti na ya kudumu kwa uaminifu.
- Kuheshimu wazazi: Watoto walifundishwa kuheshimu na kutii wazazi na wazee wao. Heshima kwa wazazi ni kanuni ya kimaadili. Katika ndoa, watoto wanaheshimiwa na kutoa kipaumbele kwa malezi yao ni sehemu ya maadili. Wazazi wanatarajiwa kuwajibika kikamilifu katika kulea watoto wao. Watoto walifundishwa utamaduni, mila, na desturi za kabila lao kama sehemu ya maadili ya malezi.
- Chakula katika familia: Watu walifundishwa kugawana chakula na kuwa wakarimu kwa wageni. Chakula ilikuwa ni njia ya kuonyesha ukarimu na ushirikiano. Pia wakati wa kula, wanafamilia walikuwa na utamaduni wa kula pamoja kama sehemu ya kutunza maadili ya Kitanzania.
- Malezi na Makuzi: Malezi yalitolewa kulingana na mila, desturi na maadili ya jamii zilizotumika. Malezi yalitolewa tangu mimba ilipotungwa, moto alipozaliwa hadi alipofikisha umri wa kuvunja ungo au kubalehe na kutambulika kama mtu mzima. Malezi hayo yalilenga aina ya vyakula; mathalani, anavyopaswa kula mama mjamzito na vitu vya kufanya ili kupata moto mwenye afya bora na salama. Malezi na makuzi ya moto pia yalitolewa ili kumjenga moto katika maadili na tabia njema katika jamii. Kwa mfano, katika jamii za Wabantu kama vile Wazaramo na Wamakonde, jando ilihusisha vijana wenye umri maalumu, mara nyingi baada ya balehe. Jandoni, vijana walipewa elimu maalumu ili kuwaandaa kuwa na maadili mema katika jamii na baba bora katika familia na viongozi katika ukoo. Vilevile, elimu ya unyago ilitolewa kwa wasichana ili kuwaanda kwenye maisha ya ndoa na kuwa mama bora wa kusimamia familia vizuri. Familia na koo zilikuwa ndiyo kitovu cha malezi na kujenga maadili katika jamii. Aidha, jamii nzima ilihusika katika makuzi ya moto na ilitambua na kuthamini jukumu la kuandaa na kukuza watoto wote kuendana na maadili ya jamii iliyohusika. Vilevile, watu walitarajiwa kuvaa kwa heshima na kujistahi, hasa katika hafla za kijamii na kidini.
-
Miiko katika Jamii: Hili ni jambo ama kitu kinachozuiwa kisifanywe kwa kuchelea kutokea madhara fulani. Kwa mfano, katika jamii nyingi zilizojihusisha kufua chuma kulikuwepo na mwiko ulionzuia mwanamke aliyekuwa kwenye hedhi kushiriki katika kazi yoyote ya kuzalisha chuma. Iliaminika kuwa akifanya hivyo basi kutatokea madhara fulani katika kazi hiyo, kama vile tanuu kupasuka wakati wa kazi ama chuma kugeuka lombwe na pengine hata wafanyakazi kupata ajali ya kuungua ama kufariki.
Mara nyingi miiko katika hizo iliendeshwa kwa imani hasa kwa vile hazitolewi sababu ama maelezo bayana yenye kuonyesha uhusiano uliopo kati ya kile kinachokatazwa na madhara yanayosemekana yatatokea endapo mwiko utavunjwa. Lakini ieleweke kuwa miko karibu yote haikuzushwa tu katika jamii. Kulikuwepo na sababu maalumu zilizosababisha jamii hizo kubuni mwiko fulani hata kama elimu na utamaduni wa leo hauoni maana yoyote katika mwiko huo.
Kwa maana hiyo, jamii ya leo inapokosa maelezo thabiti ama mantiki ya mwiko fulani isichukuliwe kuwa hao walioubuni mwiko huo walikuwa wapumbavu, bali ni matokeo ya kupita kwa wakati kwani "Wakati Ukuta". Miiko mingi katika jamii za asili ya Kitanzania, zilirithiwa katika jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Jinsi muda ulivyopita ndivyo maelezo ya kina kuhusu mwiko fulani ulivyozidi kupungua mwishowe siyo ajabu kukuta jamii ikafikia pahala ikasema "ni mwiko kuuliza sababu za mwiko".
Maadili haya ni muhimu katika kudumisha utambulisho wa Kitanzania na kujenga mahusiano yenye thamani ndani ya jamii husika.
Maadili ya Asili ya Jamii za Kitanzania Katika Nyanja za Kijamii
Mfumo wa maadili ya jamii za asili ya Kitanzania katika nyanja ya kijamii ulihusisha masuala ya elimu na maarifa, tiba na imani. Aidha, ulizingatia heshima kwa wazee wenye maarifa, utunzaji wa tamaduni na mila za tiba na ushirikiano katika masuala ya kidini. Maadili haya yalikuwa sehemu muhimu ya kudumisha utamaduni na maisha ya jamii za Kitanzania wakati wa mfumo wa kijadi wa kiutawala. Mambo haya yalisisitizwa na kufuatwa katika jamii za asili ya Kitanzania ili kudumisha mila na desturi.
Elimu na Maarifa
Ilikuwa ni wajibu wa kila jamii kutoa elimu kulingana na maadili ya jamii husika. Kwa mfano, katika jamii zote za asili, elimu ilitolewa katika ngazi ya familia kwa njia ya vitendo. Watu wazima, watu rasmi na wazee waliheshimiwa sana katika jamii za Kitanzania kwa sababu wengi wao walikuwa na jukumu la kuelimisha na kusambaza maarifa kwa vizazi vijavyo. Kizazi kipya kilipaswa kujifunza kutoka kwa wazee na wataalam wa jamii ili kuhifadhi na kuendeleza maarifa ya kale.
Kwa mfano, katika jamii za Wakichembe, kijana alifundishwa kuwinda kwa kuambatana na watu wazima wakati wa mawindo. Vijana walifundishwa dawa za asili kwa kuwaangalia wazazi wao wanatumia mti gani pale wanapougua. Vilevile, vijana walifundishwa maarifa na maadili mbalimbali kuhusu vita, uwindaji, tiba asili, uhunzi, ufinyanzi, imani za jadi, na historia ya jamii katika makundirika, nyumbani na katika sherehe za jando na unyago. Elimu iliyotolewa ililenga:
- Kujikinga na kutibu maradhi mbalimbali ya binadamu na wanyama
- Kuhimiza tabia ya ushirikiano, utu, undugu na upendo
- Kusisitiza tabia ya kuheshimu utu na kufuata utaratibu
- Kujilinda na majanga mbalimbali katika jamii
- Kuenzi na kuendeleza mila, desturi na taratibu za jamii zilizohudumishwa
Tiba za asili
Kwa tafsiri ya jumla ya jadi za Kiafrika, dawa ni kitu chochote, kiwe katika hali inayogusika na isiyo gusika, kinachotumika kwa malengo ama mazuri, kama vile kutibu na kukinga au malaya, kama vile kuua na kuroga. Matibabu hayo au kinga hizo zinaweza kumhusu binadamu mmoja ama kundi, iwe katika mwili wake, matendo yake ama mali zake. Mwili hutibiwa magonjwa ama hukingwa usipatwe na magonjwa au madhara mengine.
Katika jamii za asili ya Kitanzania matendo kama vile uvuvi, kilimo, ufundi, na kadhalika yalitibiwa na kufanyiwa kwa kutumia dawa maalumu pale ilipoonekana dalili za kupungua au kukosekana kabisa kwa mapato. Matendo hayo pia yalikingwa ili yasipatwe na mabalaa au ajali yoyote. Mali kama vile mimea, wanyama, ardhi, maji, nyumba, na kadhalika yalitibiwa na kukingwa dhidi ya maradhi na uharibifu mbalimbali.
Dawa ziliweza pia kutumiwa kwa nia mbaya hasa katika mambo yaliyoendana na wivu. Katika jamii hizo, pia dawa zilizotumiwa na wachawi, imani ambazo ziliota mizizi katika mila na desturi za Kitanzania.
Wachawi waliaminika kuwa na dawa zenye uwezo wa kuroga mathalani, vitendeakazi - jembe, nyavu, bunduki, gari, nyumba ya biashara, shamba, na kadhalika - visiweze kufanya kazi ipasavyo na hivyo kuathiri tija ya majirani zao. Kwa imani hii, tanuu la kuzalishia mali pia liweza kuathiriwa na dawa za kichawi.
Tiba za asili ilikuwa ni sehemu muhimu ya utamaduni na mfumo wa afya katika jamii za asili ya Kitanzania. Mimea mingi ilitumiwa kama tiba za asili. Wazee na wataalamu wa tiba ya jadi walijua jinsi ya kutambua mimea inayotumika kutibu magonjwa mbalimbali. Kwa mfano, mmea wa mlonge ulitumiwa kutibu malaria, mmea wa mdalasini ulitumika kutibu magonjwa ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula. Zipo jamii zilizotumia asali, mafuta ya mimea na mchanganyiko wa viungo vingine vya asili kama vile vitunguu na tangawizi kutibu magonjwa.
Imani na dini
Imani na dini katika jamii za kale zilijengeka katika misingi ya mila na desturi ya jamii iliyohusika. Watu waliamini uwepo wa Mungu na mizimu na kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu na mtawala wa vitu vyote. Imani hizo zilisababisha watu kumfananisha Mungu na miungu au vitu vikubwa katika ulimwengu kama vile jua, milima, mito na misitu mikubwa.
Watu waliamini kuwa Mungu ndiye anayetawala kila kitu na mwenye mamlaka ya mwisho kwa kila jambo kama vile mabadiliko ya tabianchi na maisha ya viumbe vyote. Jamii pia zilifundishwa na kuaminishwa katika imani za jamii zao. Jamii zilikuwa na utaratibu wake wa kufanya ibada. Ibada hizo ziliitwa matambiko ambayo yalifanyika katika maeneo mbalimbali kama vile makaburini, kwenye miti mikubwa, milimani, misituni, mapangoni, njiapanda, ziwani, baharini na kwenye mawe makubwa kutegemeana na aina ya matambiko.
Kwa mfano, msitu wa Nyumbanitu mkoani Njombe ni moja ya maeneo maarufu ya ibada za matambiko. Madhumuni ya matambiko hayo pamoja na kupeleka maombi kwa Mungu kupitia mizimu ili kupata baraka, mvua, mavuno na pengine kuondoa mikosi au majanga katika jamii. Jamii hizi pia ziliabudu kupitia mizimu ya kale. Watu walitoa sadaka wakati wa ibada kama vile wanyama, pombe na nafaka na kufanya matambiko kama sehemu ya maadili. Matambiko hayo yaliongozwa na wazee au viongozi wa koo.
Jamii za asili za Tanzania ziliamini kutokufanya ibada kungesababisha matatizo na madhara katika jamii. Mambo mabaya kama vile, majanga yalipotokea jamii ziliamini ni kutokana na kutofanya ibada. Maadili kuhusu imani na dini katika jamii yalirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Aidha, katika jamii nyingine, matambiko yalihusisha sherehe za kimila kwa lengo la kutimiza ibada na kuwafunza watu maadili ya jamii iliyohusika kama sehemu ya ibada. Kwa mfano, miti mikubwa ya asili na misitu minene ilitumika kwa matambiko na haikuruhusiwa mtu kuingia bila ruhusa maalumu. Lengo liikuwa kutunza na kuhifadhi mazingira. Pia, watu waliaswa kutimiza na kufuata taratibu za ibada ili kuepuka kupata mikosi na balaa.
Vilevile, imani za dini ziliambatana na matumizi ya dawa za asili ili kukinga na kutibu magonjwa na maradhi mbalimbali. Huduma hii ilitolewa na wazee wa kimila, waganga na wakunga wa jadi kwa kutumia mitishamba na dawa zingine. Aidha, waganga na wanawake hawa wa kila walifanya matibabu kwa kutegemea ibada za mizimu na ramli.
Kwa ujumla, watu walipaswa kuheshimu na kushiriki katika ibada na mila za kidini. Ibada na shughuli za kidini zilikuwa njia ya kuleta umoja na ushirikiano katika jamii. Watu walipaswa kushiriki kwa dhati katika shughuli za kidini.
Kufanya mazindiko
Zindiko ni fingo, yaani dawa maalumu zinazoaminika kuwa na uwezo wa kukinga kitu kinachozindikwa kisipatwe na madhara, hususani yatokanayo na uchawi. Katika jamii za asili ya Kitanzania, mara nyingi uzindikaji ulifanywa katika vitendeakazi kama vile bunduki, shoka, jembe, nyavu, ngalawa, na magari; wanyama wazalishaji kama vile binadamu, mbwa wa msasi, ngombe, na punda; majengo iwe ya kukaa, yaani nyumba, ama yale ya kufanyia biashara mathalani maduka, na ya ibada, kama vile kwenye mawe makubwa, misitu minene au hata mapangoni kadhalika.
Kila zindiko liikuwa na lengo maalumu. Kwa mfano, watu walizindika mali yao dhidi ya maradhi ya kurogwa; nyumba ya makazi yalizindikwa ili wale wenye makusudi ya kuwadhuru wakazi wake wasifanikive; mashamba yalizindikwa ili mazao yake yasiibwe kiuchawi. Kwa ujumla, tanuu ya uzalishaji mali yalizindikwa ili kazi isiharibiwe na wachawi na kadhalika.
Katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknologia, zindiko linaweza kulinganishwa kama chanjo za kinga, mathalani za magonjwa kama vile ndui, surua, pepopunda, na nyinginezo ambazo humzuia yule aliyechanjwa asifikwe na maradhi hayo kiurahisi.
Maswali ya Kujipima
Jibu maswali yafuatayo:
-
Katika jamii za Kitanzania, ni vipi ushirikiano na umoja huchangia katika kusuluhisha migogoro ya kijamii na kuleta maendeleo endelevu?
-
Taratibu gani za utamaduni na mila zinazoheshimiwa katika jamii za Kitanzania na ni kwa namna gani zinaunganisha watu kijamii?
-
Kwa nini uwajibikaji ni muhimu katika jamii za Kitanzania na ni jinsi gani watu hutekeleza majukumu yao kwa uaminifu katika muktadha wa kijamii?
-
Toa mifano ya jinsi adabu na heshima kwa wengine zinavyopewa kipaumbele katika mawasiliano ya kijamii ya Kitanzania.
-
Eleza namna jamii za Kitanzania huonesha kujali na kusaidia watu wanyonge au wenye mahitaji katika muktadha wa kijamii.
-
Eleza jinsi maadili kuhusu imani na dini yalivyokuwa yakirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine katika jamii za asili za Tanzania.
-
Toa mifano ya tabia za kuheshimu na kujali utu wa mtu mwingine kutoka katika jamii za asili.
-
Fafanua malengo ya ujenzi wa maadili katika jamii za asili za Kitanzania.
-
Eleza tofauti iliyopo kati ya maadili yaliyojengwa katika jamii za asili na jamii za sasa za Kitanzania.
-
Ni maadili gani ya jamii za asili yanayopaswa kuendelezwa ili kukuza na kujenga maadili katika jamii za sasa za Kitanzania?
Maadili ya Jamii za Asili ya Kitanzania Katika Nyanja za Kisiasa (Mfumo wa Kiutawala)
Maadili ya jamii za asili ya Kitanzania katika nyanja ya siasa ilihusisha mifumo ya kiutawala wa jamii husika. Aidha, mifumo hiyo ilitofautiana baina ya jamii moja na nyingine kulingana na tamaduni za jamii husika. Sifa mojawapo ya kuwa kiongozi katika jamii za asili ya Kitanzania ilikuwa pamoja na kumkakamavu, hodari na jasiri. Kwa ujumla, maadili katika jamii hizi yalisistitza mambo yafuatayo:
- Kufanya kazi kwa uadilifu na kujali wengine. Katika mfumo wa kale, uwazi na uwajibikaji kwa viongozi na wanajamii wenyewe ilikuwa jambo la muhimu sana. Viongozi wa koo na kaya zake walisisitiza uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii kwa kila mwanajamii. Viongozi wa koo mbalimbali walifanya maamuzi yao kwa uwazi na kwa manufaa ya jamii. Kwa upande mwingine, maamuzi yalipaswa kuwa ya haki. Viongozi walipaswa kuwa waadilifu katika utawala wao. Vilevile, mfumo wa kale/asili ulihimiza uvumilivu na amani. Migogoro ilipaswa kutatuliwa kwa njia ya amani.
- Viongozi wa jamii mbalimbali kama vile wakuu wa koo walisisitizwa kuwa uaminifu na kuwahesimu wale wanaowaongoza. Uaminifu na heshima vilichukuliwa kuwa mojawapo ya maadili muhimu zaidi katika maisha ya jamii husika. Pia, kiongozi alitakiwa kuwa na uwezo wa kuzingatia ahadi na majukumu yake, kuheshimu haki za wengine, na kuthamini tofauti na maoni ya wanajamii anaowaongoza.
- Kuheshimu mila, desturi na utamaduni. Utamaduni na mila za kabila ziliheshimiwa na zilikuwa sehemu muhimu ya uongozi wa kijadi. Viongozi walipaswa kuheshimu na kusimamia mila za kitamaduni.
- Vijana na viongozi wote walihimizwa kubeshimu wazee wa kijadi. Wazee hawa walikuwa na nafasi ya heshima katika uongozi wa kijadi. Walikuwa washauri na wenye hekima katika kufanya maamuzi. Wazee wa kijadi waliheshimiwa kwa busara na hekima yao.
- Jamii za Kitanzania zilendeshwa kwa misingi ya ushirikiano na umoja. Ushirikiano ulijikita katika mambo yote ya furaha na huzuni, kama vile harusi na misiba. Aidha, viongozi walisikiliza maoni ya wanajamii na kufanya maamuzi kwa kushirikiana. Pia, familia na jamii nzima zilikuwa na jukumu muhimu katika uongozi wa kijadi. Ushirikiano na kusaidiana vilikuwa sehemu ya maadili na kanuni muhimu kwa maisha ya kila siku. Watu wote walipaswa kubeshimiwa bila kujali hali zao za kijamii au kiuchumi.
Kwa ujumla, maadili haya yalikuwa na ni muhimu hata sasa katika kudumisha utulivu na ufanisi katika jamii za Kitanzania.
Maadili ya Jamii za Kitanzania Katika Nyanja ya Kiuchumi
Mfumo wa maadili ya jamii za Kitanzania katika uchumi ulihusisha kilimo, biashara na vivanda. Katika kutekeleza shughuli katika nyanja ya kiuchumi, maadili yalionekana katika maeneo yafuatayo:
- Ushirikiano katika uzalishaji mali: Jamii za Kitanzania zilithamini ushirikiano katika shughuli za kiuchumi. Kwa mfano, familia au kaya moja ilishirikiana na nyingine kuzalisha mali kama vile kufanya kilimo cha mazao. Zipo pia jamii zilizoshirikiana katika shughuli za ujenzi. Baada ya uzalishaji kuongezeka, jamii nyingi zilishirikiana katika biashara. Biashara ya kijadi kama vile ubadilishaji wa bidhaa kwa bidhaa na biashara za kienyeji zilikuwa sehemu muhimu ya maisha ya kiuchumi. Watu waliheshimu makubaliano na taratibu za biashara hizi. Watu walikuwa waadilifu na kuheshimu makubaliano katika biashara walizofanya. Udanganyifu na ulaghai katika biashara vilichukuliwa kuwa kinyume cha maadili.
- Uzalishaji wa kujitosheleza: Jamii za Kitanzania zilitilia mkazo uzalishaji wa kujitosheleza, hasa katika kilimo. Kilimo kilikuwa shughuli kuu ya kiuchumi na familia zilitegemea kujitosheleza kwa chakula na mahitaji mengine ya kila siku. Matumizi ya ardhi yalifanywa kwa uangalifu ili kuhakikisha hakuna migogoro baina ya jamii moja na nyingine.
- Sanaa na Ufundi: Sanaa na ufundi wa kitamaduni viliheshimiwa na kuthaminiwa. Watu walipaswa kuhifadhi na kukuza ujuzi wa kisanii na ufundi. Mfano, sanaa za uchongaji na ugunduzi wa teknologia za metall.
Maswali ya Kujipima
-
Toa mifano ya tabia za kuheshimu na kujali utu wa mtu mwingine kutoka katika jamii za asili.
-
Eleza tofauti iliyopo kati ya maadili yaliyojengwa katika jamii za asili na jamii za sasa za Kitanzania.
-
Maadili katika jamii za asili yaliendelezwa ili kukuza na kujenga maadili katika jamii za sasa za Kitanzania. Jadili kauli hii
-
Fafanua mchango wa maadili katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika jamii za sasa za Kitanzania.
-
Bainisha changamoto za kukuza maadili katika jamii unamoishi na kisha toa mapendekezo ya jinsi ya kuzitatua.

No comments
Post a Comment