NUKUU ZA KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA

Sura ya Kwanza: Lugha na Utamaduni

Sura ya Kwanza: LUGHA NA UTAMADUNI

Utangulizi

Mawasiliano hufanyika miongoni mwa wanajamii kupitia lugha. Aidha, watu wenye utamaduni mmoja hutambulika kupitia lugha wanayoitumia. Katika sura hii, utajifunza namna Kiswahili kinavyofungamana na jamii na utamaduni. Vilevile, utajifunza namna Kiswahili kinavyoweza kutumika kama kielelezo cha utamaduni wa Mtanzania pamoja na umuhimu wa kujifunza Kiswahili.

Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuwasiliana kwa kutumia Kiswahili fasaha katika miktadha mbalimbali kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania. Pia, utaweza kujenga tabia ya udadisi na ubunifu katika masuala mbalimbali ya lugha ya Kiswahili na matumizi yake.

Fikiri: Lugha na utamaduni vinavyohusiana

Matumizi ya lugha ya Kiswahili kama utambulisho wa Mtanzania

Soma habari kuhusu Kijiji cha Safina, kisha jibu maswali yanayofuata.

Kijiji cha Safina kilikuwa na wakazi wenye makabila anuai. Wakazi wa kijiji hicho hawakuweza kuwasiliana kwa sababu walitumia lugha tofauti. Mwaka fulani kulttokea ukame katika kijiji hicho, hali iliyodumu kwa muda mrefu. Kutokana na hali hiyo, iliwalazimu wanakijiji hao kuhamia karibu na chanzo cha maji ili waveze kupata huduma ya maji. Wanakijiji hao walikaa kwa pamoja kwa kipindi chote cha ukame, hali iliyofanya kuwa na msamiati unaofanana kutokana na baadhi ya maneno kutumika mara kwa mara miongoni mwao.

Baada ya muda kupita, wanakijiji hao walijikuta wana mfumo mmoja wa mawasiliano ambao ulieleweka miongoni mwa wanakijiji wote. Kuanzia hapo, watu wa Kijiji cha Safina wakakubaliana kutumia mfumo huo wa mawasiliano. Muda ulivyozidi kwenda, walijikuta wanaujua na kuutumia mfumo huo bila mafunzo rasmi. Mfumo huo ulioibuka kinasibu ulikuwa na mpangilio maalumu wa sauti, silabi, maneno na sentensi ambao unaleta maana. Waliendelea kuongeza maneno katika lugha hiyo kadiri walivyokutana na dhana myya katika mazingira yao kwa kufuata mfumo wa lugha hiyo. Majina yao na ya maeneo yao yaliendana na maana na dhana kama zilivyokubaliwa katika jamii yao. Hivyo, maana za maneno yao zilitambulisha jamii yao kupitia mfumo wao wa mawasiliano.

Aidha, mfumo huo uliwafanya wanakijiji hao waanze kuelewana katika mazungumzo yao na kufanya shughuli mbalimbali kwa pamoja. Walianza kuwasiliana kwa kutumia mfumo wao kwa kuzungumza kisha wakajifunza kuandika.

Wakazi wa kijiji hicho waliunganishwa pamoja kupitia mfumo huo wa mawasiliano kwani ulitumiwa na watu wote. Hivyo, jamii ya Safina haikuwa na namna nyingine ya kueleza masuala yake pasipo kutumia mfumo huo wa mawasiliano. Kwa hakika, wakazi wa Kijiji cha Safina walljenga uhusiano mzuri miongoni mwao kama wanajamii moja.

Sanjari na hayo, mfumo wa mawasiliano wa Kijiji cha Safina uliwavezesha wanakijiji hao kufikiri, kuhifadhi na kurithisha maarifa na amali zao kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Vilevile, kupitia mfumo huo wa mawasiliano, watu wa kijiji cha Safina waliweza kutambulika kila walipokwenda kwani waljitofautisha na wazungumzaji wa mahali pengine kutokana na uzungumzaji wao.

Pia, waliweza kuendeleza utamaduni wao na kuongeza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia mfumo wa mawasiliano walioutumia. Hivyo, Kijiji cha Safina kilifanikiwa kukua na kuwa na maendeleo makubwa sana.

Maswali

  1. Unafikiri mfumo uliotumiwa na wanakijiji wa Safina katika kuwasiliana unaitwaje?
  2. Umejifunza nini kuhusu dhana ya lugha kutokana na habari uliyoisoma?
  3. Vipengele gani vya lugha hujenga mpangilio wa mfumo wa mawasiliano kwa mujibu wa habari uliyoisoma?
  4. Kuna uhusiano gani kati ya lugha na jamii kulingana na habari uliyoisoma?
  5. Kutokana na habari uliyoisoma, lugha ina dhima zipi?

Zingatia

Lugha ni mfumo au mpangilio maalumu wa sauti za nasibu wenye kuleta maana, uliokubalika kutumika katika kuwasiliana miongoni mwa wanajamii wenye utamaduni mmoja. Mfumo huo unahusisha kipengele cha sauti, silabi, maneno, sentensi na maana. Sauti katika maneno na maneno katika sentensi hupangwa kwa utaratibu maalumu kulingana na lugha inayohusika ili kuleta maana. Hivyo, mpangilio huo hutofautisha lugha moja na nyingine.

Lugha na jamii hufunganana kwa kuwa lugha ndiyo huwavezesha wanajamii kufahamiana, kubadilishana mawazo, kupashana habari, na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii. Aidha, lugha hukua kadiri inavyotumika katika shughuli hizo anuai za kijamii. Sanjari na hayo, maana na dhana mbalimbali zinazobebwa na maneno ya lugha hutokana na utamaduni wa jamii inayohusika pamoja na mazingira yao. Kwa hiyo, lugha ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano katika jamii yenye utamaduni mmoja. Aidha, lugha hukua kadiri inavyotumiva na hufa isipotumiva. Vilevile, kila lugha inajitosheleza katika mawasiliano ya jamii husika kwa sababu huweza kueleza yaliyopo, yaliyopita, yajayo na yanayofikirika.

Shughuli ya 1.1

Fikiria umeshiriki katika kongamano linalowahusisha wanafunzi wenye tamaduni tofauti na utamaduni wako. Je, utatumia vipengele gani vya lugha kuutambulisha utamaduni wako?

Hadhi ya Kiswahili

Soma shairi lifuatalo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Nataka nena na wewe, upate kunielewa,

Wengi washikwa kiwewe, kwa kushindwa nielewa,

Yapaswa unielewe, nimekwishakubaliwa,

Sauti zangu nasibu, hakuna wa kukanusha,

Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda.

Huwezi kuwazuia, waliokubaliana,

Mimi wanantiumia, wapate kuelewana,

Kanuni wazingatia, ili kuwasiliana,

Malengo pate fikia, wote kushirikiana,

Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda.

Majina pia mavazi, vyote vyantiegemea,

Shughuli jamii hizi, lugha hii zatumia,

Kiswahili ni mzizi, kuunganisha jamia,

Ondokana na simanzi, kubali kunitumia,

Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda.

Mimi nimekubalika, katika hii dunia,

Rasmi ni kutumika, kote kule Tanzania,

Duniani na Afrika, nimeweza kuendelea,

Kiswahili chasifika, lugha ya kinataifa,

Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda.

Maswali

  1. Shairi ulilolisoma linazungumzia nini?
  2. Sifa gani za Kiswahili zimebainishwa katika shairi hilo?
  3. Unafikiri Kiswahili kina sifa gani nyingine tofauti na alizozieleza mwandishi?
  4. Mstari unaosema, "Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda" una maana gani?

Zoezi la 1.1

  1. Fafanua mawazo makuu mawili yaliyowasilishwa katika ubeti wa pili wa shairi ulilolisoma.
  2. Eleza hadhi ya Kiswahili kama ilivyofafanuliwa katika shairi.

Zingatia

Nchini Tanzania Kiswahili ndiyo lugha inayotumiwa na takribani Watanzania wote. Aidha, ni lugha inayowaniganisha Watanzania wote kama lugha kuu ya mawasiliano kwa kuwa hutumika katika shughuli kama vile; za kijamii za kila siku, za kiserikali, kisiasa, kidini na kibiashara. Pia, hutumika kutaja majina ya vitu vinavyowazunguka wasemaji wake na masuala mbalimbali ya utamaduni wao kama vile vyakula na mavazi. Vilevile, hutaja majina ya watu, mathalani; Pili, Lukasa, Juma, Furaha, Upendo na Amani. Hivyo, lugha ya Kiswahili ni utambulisho wa Mtanzania.

Matumizi ya lugha ya Kiswahili kama kielelezo cha utamaduni wa Mtanzania

Soma dayolojia ifuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Bibi:
Hamjambo wajukuu zangu?
Wajukuu:
Hatujambo. Shikamoo bibi.
Bibi:
Marahaba wajukuu zangu. (Anatiikia akiwa anatabasamu.)
Wajukuu:
Bibi …! Tumeshamaliza kula, tumeshaosha vyombo, sasa tuko tayari kukusikiliza ili utueleze kuhusu maadili ya Watanzania kama ulivyotuahidi jana.
Bibi:
Hahaaaa! Wajukuu zangu hamjasahau? (Aliuliza.)
Wajukuu:
(Walijibu kwa pamoja.) Hatujasahau bibi.
Bibi:
Sawa! Na mimi niko tayari kuwaeleza kuhusu suala hilo.
Wajukuu:
Sawa bibi … (Huku wakijiweka tayari kusikiliza.)
Bibi:
Maadili ni suala muhimu kwa kila jamii. Kila jamii inatakiwa kuzingatia maadili kulingana na mila na desturi za jamii husika. Wakubwa kwa wadogo, wote wanatakiwa kuheshimiana na kuthaminiana. Mila na desturi za jamii hurithishwa na kuenziwa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine. Hata ninyi wajukuu zangu mnapaswa kuishi kulingana na mila na desturi zetu.
Mjukuu wa 1:
Mh! Kwani bibi tunatakiwa tufanyeje ili tuwaheshimu wengine?
Bibi:
Swali zuri mjukuu wangu. Watoto wanatakiwa kuwaheshimu wakubwa. Mdogo akikutana na mkubwa, mdogo huanza kumsalimia mkubwa. Hata watu wa rika moja wanapokutana wanatakiwa kusalimiana kwa salamu inayoendana na rika lao. Kwa hiyo, salamu hutofautiana kulingana na rika.
Mjukuu wa 2:
Sasa bibi …! Kwa nini salamu zinatofautiana? Salamu si salamu tu?
Bibi:
Swali zuri sana. (Bibi alisema huku akitabasamu.) Salamu ni utaratibu ambao watu wamejiwekea na kukubaliana kuutumia kama sehemu ya maisha yao.
Mjukuu wa 3:
Ahaaa, kumbe …! Bibi, je kama wanatofautisha salamu, hutofautisha na maneno ya kutumia?
Bibi:
Wajukuu zangu mu wadadisi sana. (Alisema huku akitabasamu.) Ndiyo! Katika kutumia lugha, kuna miiko katika matumizi ya baadhi ya maneno. Lengo la miiko hiyo ni kuleta heshima katika mazungumzo miongoni mwa wanajamii. Kuna baadhi ya maneno ambayo huwezi kuyatamka waziwazi. Pia, katika lugha yetu ya Kiswahili kuna utajiri huo wa kiutamaduni. Hivyo, katika mila na desturi zetu, hatutamki baadhi ya maneno waziwazi. Kwa mfano, mwanamke anapopata moto hatusemi amezaa moto badala yake tunasema amejifungua. Vilevile, mtu anapokwenda chooni, badala ya kusema kile anachotaka kwenda kufanya huko anasema ninakwenda kujisaidia au ninakwenda haja.
Mjukuu wa 4:
Bibi, maneno hayo yalitamkwa kwa kificho tangu zamani?
Bibi:
Ndiyo mjukuu wangu. Mila na desturi zinarithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Kiswahili kimesheheni maneno hayo ya kificho ambayo hujulikana kama tafsida.
Mjukuu wa 4:
Ahaaa! Sasa nimeelewa.
Mjukuu wa 5:
Bibi, hivi mtu akiumwa au kupatwa na matatizo tunatakiwa tufanyeje?
Bibi:
Swali zuri mjukuu wangu. Kwa hakika, tunapaswa kuishi kwa kujaliana na kufarijiana. Kujaliana na kufarijiana huonesha hali ya kuthaminiana. Kwa mfano, mtu anapougua au kupata changamoto yoyote ile katika jamii yetu, lugha yetu ina maneno kama vile pole ambayo hutumika katika kumfariji. Pia, katika kuonesha kujaliana, maneno kama asante na shukurani hutumika pale mtu anapokupa kitu au msaada fulani. Aidha, unapotaka kuomba kitu au msaada fulani sharti kutumia maneno yanayoonesha upole. Maneno hayo ni pamoja na samahani, tafadhali, ninaomba na mengine yanayofanana na hayo.
Mjukuu wa 1:
Kwa kweli leo nimelifunza mambo mengi kuhusu utamaduni wetu, hususani kuhusu maadili. Ninatamani uendelee kutueleza mengine zaidi.
Bibi:
Safi! Ngoja nivajuze mengine wajukuu zangu. Katika maisha ni muhimu kusaidiana. Ikitokea mdogo amekutana na mkubwa akiwa na mzigo, mdogo anapaswa kumsaidia mkubwa kubeba mzigo huo. Hata hivyo, si wadogo tu wanaotakiwa kuwasaidia wengine; hata watu wazima husaidiana. Hii ni alama ya ukarimu. Ukarimu ni sifa muhimu sana kwa kila Mtanzania.
Mjukuu wa 1:
Bibi …! Inaonekana katika lugha kuna hazina kubwa sana ya utamaduni wetu.
Bibi:
Kabisa! Kabisa! ... (Bibi alivuta pumzi kidogo.) Kwa mfano, Lugha ya Kiswahili ni alama ya utambulisho wa utamaduni wetu. Kupitia lugha yetu ya Kiswahili tunaweza kuutambua, kuutunza na kuurithisha utamaduni wetu. Wageni pia hutambua utamaduni wetu kupitia lugha yetu.
Mjukuu wa 1:
Bibi, leo umetufundisha mambo mengi sana. Tumejua namna utamaduni na lugha vinavyofungamana. Pia, tumejua namna lugha yetu ya Kiswahili ilivyo kielelezo cha utambulisho wa utamaduni wa Mtanzania.
Bibi:
Yapo mambo mengi yanayohusiana na lugha yetu ya Kiswahili na utamaduni wetu. Haya machache yanatosha kwa leo. Siku nyingine nitawaeleza mambo mengine yanayohusu lugha yetu. Twendeni tukalale ili kesho muweze kuwahi shuleni.
Wajukuu:
Asante bibi. Kwaheri. (Wanaondoka kwenda kulala.)
Bibi:
Kwaherini wajukuu zangu.

Maswali

  1. Dayolojia uliyoisoma inahusu nini?
  2. Kutokana na dayolojia uliyoisoma, kwa nini tunatumia tafsida?
  3. Kwa nini ni muhimu kuishi kwa kufuata mila na desturi za jamii husika?
  4. Utamaduni hurithishwa kwa njia gani?
  5. Umejifunza nini kutokana na dayolojia uliyoisoma?

Shughuli ya 1.2

Kusanya vitu mbalimbali yenye maandishi ya lugha ya Kiswahili, kama vile misemo katika kawa na kanga, vinavyoweza kutambulisha utamaduni wa Mtanzania na kueleza namna lugha iliyotumika inavyotambulisha utamaduni wa Mtanzania.

Zingatia

Utamaduni ni mfumo wa maisha ambao watu wa jamii fulani wamejiwekea katika kuendesha maisha yao ya kila siku. Lugha ni miongoni mwa vitambulisho vya utamaduni wa jamii husika. Mathalani, utamaduni wa Mtanzania huweza kutambulishwa na lugha ya Kiswahili. Hii hudhihirika katika mambo mbalimbali ambayo hufanywa na Watanzania kama sehemu ya utamaduni wao kupitia lugha ya Kiswahili. Aidha, vipengele mbalimbali vya kiutamaduni huelezwa kwa lugha; mathalani, majina ya vyakula. Vilevile, matumizi ya maneno ya lugha na maana zake hufungamana na utamaduni. Hivyo, lugha ni chombo na nyenzo inayobeba utamaduni wa wazungumzaji wa lugha husika.

Shughuli ya 1.3

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, vikiwemo vya mkondoni vinavyoaminika, sikiliza masimulizi yenye maudhui ya utamaduni wa Mtanzania, kisha bainisha vipengele vya utamaduni vilivyobainishwa.

Umuhimu wa kujifunza Kiswahili

Soma mahojiano baina ya Mwandishi wa habari na Mwalimu, kisha jibu maswali yanayofuata.

Siku moja, mwandishi wa habari alifanya mahojiano na Mwalimu wa somo la Kiswahili kuhusu umuhimu wa kujifunza Somo la Kiswahili. Katika mahojiano hayo, mambo mbalimbali yalizungumziwa ambayo ni zao la kujifunza Somo la Kiswahili. Mahojiano hayo valikuwa kama ifuatavyo:

Mwalimu:
Habari ndugu mwandishi!
Mwandishi:
Nzuri mwalimu.
Mwalimu:
Karibu sana.
Mwandishi:
Asante. Mwalimu, baadhi ya watu hawaoni umuhimu wa kujifunza Kiswahili. Wewe una maoni gani?
Mwalimu:
Kwa kweli, hayo ni mawazo potofu. Tuelewe kuwa lugha ya Kiswahili nehini Tanzania hutumika kufundishia masomo yote katika shule za msingi na vyuo vya ualimu vinavyotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia. Pia, Kiswahili hufundishwa kama somo katika elimu ya sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu. Hii ina mchango mkubwa sana kwa wajifunzaji kwani inawasaidia kuwa mahiri katika lugha ya Kiswahili.
Mwandishi:
Mbali na umuhimu huo, kuna umuhimu mwingine?
Mwalimu:
Ndiyo. Lugha ya Kiswahili inatumika kuwaunganisha Watanzania wote. Tanzania inakadiriva kuwa na watu zaidi ya milioni sitini wenye makabila tofauti lakini wanaunganishwa na lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao. Aidha, Kiswahili kinachangia katika kukuza uchumi, amani, na utulivu nehini Tanzania na katika nehi za jirani. Isitoshe, wakati wa kupigania uhuru, lugha ya Kiswahili ilitumika kama chombo muhimu cha umoja na mawasiliano.
Mwandishi:
Ooh! Hakika mwalimu. Kuna kingine zaidi?
Mwalimu:
Ndiyo ndugu mwandishi. Lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi pia. Inatumika katika shughuli mbalimbali za kielimu, kiuchumi na kiserikali katika taasisi na vyombo vya dola kama vile mahakama na bunge. Vilevile, Kiswahili kama lugha ya taifa hutumika kama utambulisho wa taifa letu. Kwa hiyo, Kiswahili kina nafasi kubwa katika nyanja zote za maendeleo ya taifa.
Mwandishi:
Kiswahili kina hadhi gani kimataifa?
Mwalimu:
Kiswahili kimepata hadhi ya kutumika kimataifa. Hadhi hii imekifanya Kiswahili kuwa lugha pekee ya Kiafrika iliyotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kupewa siku maalumu ya tarehe 07/07 ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani. Aidha, hii ndiyo lugha pekee ya Kiafrika ambayo imesambaa zaidi kuliko lugha zingine. Hivyo, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuleta umoja barani Afrika. Vilevile, Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika iliyopendekezwa kutumika katika vikao vya Umoja wa Afrika sanjari na lugha zingine za kimataifa. Aidha, Kiswahili kinatumika kama lugha rasmi katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mwandishi:
Ni fursa zipi ambazo Watanzania wanafaidika nazo kutokana na kupanda hadhi kwa lugha ya Kiswahili?
Mwalimu:
Kiswahili hutoa fursa za ajira; kwa mfano, baadhi ya Watanzania wenye taaluma ya kufundisha Kiswahili hujipatia fedha kutokana na kufundisha Kiswahili ndani na nje ya nchi. Aidha, kupitia taaluma ya ukalimani na tafsiri Watanzania huweza kupata ajira. Vilevile, kutokana na umuhimu wa Kiswahili kutumika nje ya nchi, baadhi ya nchi kama vile Afrika Kusini, Nigeria na Sudani Kusini zimekuwa zikihitaji wataalamu wa Kiswahili kwenda kukifundisha katika nchi hizo. Hizo zote ni fursa.
Mwandishi:
Sasa turudi kwa wanafunzi. Je, wanafunzi wanapojifunza somo la Kiswahili katika elimu ya sekondari wanapata manufaa gani?
Mwalimu:
Mwanafunzi akijifunza kikamilifu somo la Kiswahili katika elimu ya sekondari, ataweza kuwasiliana kwa Kiswahili fasaha katika nyanja mbalimbali za maisha na kukithamini Kiswahili kama sehemu muhimu ya utamaduni wa Mtanzania. Vilevile, husaidia kujenga tabia ya udadisi na ubunifu katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiswahili pamoja na kuelewa, kuthamini na kutumia kazi za fasihi katika maisha. Aidha, ataweza kutumia lugha hii katika miktadha mbalimbali, kuikuza, kuieneza na kukuza matumizi yake katika mawasiliano ya kitaifa na kimataifa. Vilevile, atajenga uwezo wa kujisomea maandiko mbalimbali ya Kiswahili. Pia, atapata msingi bora na imara wa kujifunza na kujiendeleza katika taaluma za Kiswahili kama vile uhariri, ukalimani na tafsiri na kukitumia kupata maarifa, mwelekeo, na stadi za kijamii, kitamaduni, kiteknolojia, na kitaaluma kwani lugha ni kibebeo cha maarifa.
Mwandishi:
Mwalimu, ninakupa nafasi ya kumalizia suala hili muhimu, kama una lolote la kuongezea ili tuhitimishe.
Mwalimu:
Ndugu mwandishi, ninapenda kumalizia kwa kueleza kwamba, lugha ya Kiswahili, kama zilivyo lugha zingine, inaweza kutumika kutolea maarifa na ujuzi wa taaluma mbalimbali kama vile habari na mawasiliano, historia, sayansi na teknologia. Hivyo, tuithamini na kuitumia zaidi.
Mwandishi:
Asante sana mwalimu kwa maelezo yako ya kina kuhusu umuhimu wa kujifunza Kiswahili.
Mwalimu:
Asante na karibu tena.
Mwandishi:
Shukurani.

Maswali

  1. Umejifunza nini kutokana na habari uliyoisoma?
  2. Unafikiri kuna umuhimu gani kwa mwanafunzi kujifunza somo la Kiswahili katika elimu ya sekondari?
  3. Lugha ya Kiswahili ina hadhi gani kitaifa na kimataifa?
  4. Kwa nini mwandishi alimshukuru mwalimu?
  5. Habari uliyoisoma inaeleza nini kuhusu umuhimu wa Kiswahili katika harakati za kupigania uhuru?

Zoezi la Marudio la 1

1. Jibu maswali kwa kuandika herufi ya jibu sahihi.

  1. Ipi kati ya tungo zifuatazo si dhima ya lugha katika mawasiliano?
    1. Kutambulisha utamaduni
    2. Kutumia mpangilio maalumu wa sauti
    3. Kuunganisha watu
    4. Kurithisha amali za jamii
    5. Kupashana habari
  2. Vipengele vipi vya lugha kati ya vifuataavyo hubainisha utamaduni wa Mtanzania?
    1. Unasibu, salamu, mavazi
    2. Vyakula, kilimo, mavazi
    3. Nyimbo, unasibu, mavazi
    4. Salamu, mavazi, vyakula
    5. Mavazi, unasibu, vyakula
  3. Ni jambo gani muhimu katika kufasili lugha kati ya mambo yafuataayo?
    1. Mfumo wa sauti za nasibu
    2. Mfumo wa kutamka
    3. Mfumo wa kuwasiliana
    4. Mfumo wa kuelezea matukio
    5. Mfumo wa mazungumzo ya kawaida
  4. Ipi kati ya zifuatazo ni sababu ya kuzingatia lugha na utamaduni wake?
    1. Kuweza kutamka kwa usahihi
    2. Kuweza kuwasiliana kwa usahihi
    3. Kuweza kutamka lafudhi yake kwa usahihi
    4. Kuweza kuburudika vizuri
    5. Kuweza kuunganisha watu
  5. Ipi kati ya zifuatazo ni fursa itokanayo na lugha ya Kiswahili?
    1. Kuwatambulisha watu
    2. Kuwafundisha watu wa mataifa mbalimbali
    3. Kurithisha amali za jamii
    4. Kuburudisha jamii
    5. Kuwakusanya watu katika jamii

2. Oanisha dhana zilizopo katika Orodha A na maelezo yaliyopo katika Orodha B kwa kuchagua herufi ya jibu sahihi.

Orodha A Orodha B
(i) Utambulisho wa jamii A. Tamathali ya semi inayoficha au kupunguza ukali wa neno
(ii) Tafsida B. Hueleza mambo yatokanayo na utamaduni wa Mtanzania
(iii) Utamaduni C. Upashanaji wa habari au taarifa kwa njia ya mazungumzo, maandishi na ishara
(iv) Lugha D. Makubaliano ya pamoja baina ya wazungumzaji
(v) Mawasiliano E. Mwenendo wa maisha unaohusisha asili, mila na desturi na jadi unautumika katika jamii fulani
F. Hueleza sifa bainifu za jamii fulani
G. Mfumo wa sauti za nasibu unautumia maneno yanayosemwa na binadamu ambao huwawezesha watu wa jamii fulani kuwasiliana

3. Eleza umuhimu wa kulinda na kubeshimu utamaduni wa Kitanzania.

Sura ya Pili: Sarufi ya Kiswahili

Sura ya Pili: SARUFI YA KISWAHILI

Utangulizi

Ili kuweza kuwasiliana kwa ufasaha, kanuni na taratibu zinazotawala lugha husika zinapaswa kuzingatiwa. Kanuni na taratibu hizo huhusisha matamshi sahihi, maumbo ya maneno, muundo wa tungo na maana. Katika sura hii, utajifunza vipengele hivyo vya sarufi ili kukuza uelewa wa sarufi ya Kiswahili.

Pia, utajifunza matumizi ya kiimbo, mkazo na lafudhi pamoja na mpangilio na uhusiano sahihi wa maneno katika sentensi na sentensi katika aya. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kusimulia habari na matukio kwa kuzingatia lafudhi, kiimbo na mkazo sahihi. Vilevile, utaweza kuandika matini mbalimbali kwa kuzingatia mpangilio na uhusiano sahihi wa maneno katika sentensi na sentensi katika aya.

Fikiri: Mawasiliano bila mpangilio wa maneno

Matamshi

Soma kisa kifuatacho, kisha jibu maswali yanayofuata.

Zukwe ni kijana aliyeishi katika Kijiji cha Misike kilichoko katika Wilaya ya Nduna mkoani Shobo. Kijana huyo alipenda sana kushiriki mazungumzo na vijana wenzake yaliyokuwa yakifanyika kijiweni wakati wa jioni baada ya kazi. Kijiwe hicho kiliitwa Bunguabongo kwa sababu vijana wengi waliopendelea kwenda mahali pale walikuwa wakilibua mazungumzo yaliyokuza fikra na kuwafanya wapate mwelekeo sahihi wa maisha.

Siku moja Zukwe, baada ya shughuli zake za ufugaji, alitembelea kijiweni kama ilivyokuwa ada yake. Alikwenda mahali pale kwa ajili ya kubadilishana mawazo na wenzake. Alipofika, aliwakuta vijana wenzake wakijadiliana kuhusu suala la ajira kwa vijana.

Mazungumzo yao yalikuwa hivi:

Tongoa:
Mimi ninaona ajira ziko za aina nyingi tu ila baadhi ya vijana wenzetu hawapendi kujituma; au unasemaje Benjo?
Benjo:
Kweli bwana! Kwa mfano, mimi nimeamua kujiajiri kwa kufuga kuku. Wakati ninaanza shughuli hii, vijana wengi walinidhihaki. Sasa ninaona mnanimezea mate kwa jinsi ninavyopata pesa kutokana na kuuza mayai, kuku, na mbolea inayotokana na kuku. Zukwe, si ndiyo?
Zukwe:
Haswaaa! Mimi pia nilikuwa kama wewe. Ntoto wa ndugu yangu alinicheka hivihivi kwa zarau nilipoanza kufuga mbuzi. Alisema nimekosa kazi ya kufanya. Benjo, fikiria ntoto kama yule ananicheka mimi. Ni zarau sana; ingawa sasa ninawauzia mbuzi wa nyama wafanyabiashara wa hapa kijijini na mjini.
Shehena:
Mmmh! Zukwe, umesema ntoto! Ni nani huyo? Nani anaitwa ntoto hapa kijijini? Pia, umesema zarau. Mimi sikuelewi bwana!
Chachu:
Shehena vipi? Ntoto si jina la mtu wa hapa kijijini bwana. Zukwe anamaanisha mtoto wa ndugu yake. Eti jamani … si ndivyo? (Wote wanacheka.)
Funko:
Ndivyo ilivyo Chachu. Sasa tuendelee na mazungumzo yetu. Mimi ninafikiri ajira ni tatizo. Zamani, wenzetu waliosoma walikwendaga mjini na walipata kazi lakini siku hizi wengi wanabaki hapahapa kijijini. Pia, hapa kijijini ninawapo watu wengi wanakaa tu. Ndugu zangu ajira hakuna kabisa.
Ajala:
Funko! Wanakwendaga ... ninawapo! Sema vizuri bwana. Mimi ninakubaliana na Benjo na Zukwe. Kazi za kufanya zipo nyingi. Vijana wengi tunapenda kazi za ofisini hata kama hatuna ujuzi nazo. Mtu anaweza kuajiriwa au kujiajiri kama walivyofanya wenzetu Zukwe na Benjo. Si lazima kufuga kuku tu kwani unaweza pia kujishughulisha na kilimo au biashara. Shughuli zote hizi zinaweza kutuletea maendeleo. Tufanye kazi bwana! Bila kufanya kazi maisha ni magumu mno.
Shaburi:
Kwa kweli nimejifunza jambo hapa. Kurara badala ya kutafuta kazi ya kufanya kunasababisha maisha kuwa magumu. Ama kweli erimu haina mwisho. Mazungumzo haya yamenifungua macho kabisa. Kumbe! Ninaweza kufuga, kurima au kufanya biashara nikapata kipato badala ya kuenderea kuwategemea wazazi wangu. Nadhani ningekuwa mbari kama ningeanzisha kirimo cha mbogamboga. Nani yuko tayari, tuanzishe kirimo cha mbogamboga?
Egeli:
Haaaa! Shaburi, unauliza au unaeleza? Umesahau tulivyofundishwa shule ya msingi? Kwenye swali sharti uweke kiulizo bwana.
Shaburi:
Tatizo rako wewe ni mikwara tu. Kwani hujanierewa?
Egeli:
Sema vizuri ueleweke. Mbogamboga zinalipa kweli? Mimi sina hakika. Fanya biashara ya duka Shaburi.
Shaburi:
Tatizo rako Egeri hufikirii mbari na hupendi kujishughurisha kama mimi. Mbogamboga zitaturipa sana, hasa tukirima wenyewe. Hapa kijijini maduka ni mengi tu. Tufikirie shughuri tofauti na hiyo; au mnasemaje jamani?
Zukwe, Tongoa na Benjo:
Kweli bwana.
Zukwe:
Mimi ninaweza kushirikiana na mtu yeyote anayetaka kufuga mbuzi wa nyama. Tunaweza kuwa na mradi mkubwa tukasambaza nyama katika masoko mbalimbali na kujipatia fedha. Jamani, naona Dageta hafurahishwi na mazungumzo yetu. Vipi Dageta una neno?
Dageta:
Nimehuzunika kwa sababu nimepata ujumbe wa simu wenye taharifa mbaya kutoka kwa mjomba kwamba bibi aliyemzaa mama amelazwa hospitalini.
Zukwe:
Pole sana Dageta. Ina maana umekasirika kwa sababu hiyo? Kwa nini ukasirike kama bibi yako amelazwa?
Dageta:
Du! Nimepitiva jamani. Mnajua bibi amenilea tangu nikiwa mdogo. Sijakasirika bwana.
Chachu:
Kwa hiyo, Dageta "ameluzunika." Sidhani kama unaweza kukasirika kwa sababu ya ugonjwa. Pole sana rafiki yetu.
Dageta:
Asanteni.
Zukwe:
Mazungumzo yetu yalikuwa matamu kweli lakini giza limeingia. Kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho. Kikubwa hapa ni kufanya kazi kwa bidii ndugu zangu. Tumsindikize rafiki yetu Dageta kwenda hospitalini. Mnaonaje?
Wote:
Sawa. (Wanaondoka na kwenda hospitalini.)

Wakiwa njiani kuelekea hospitalini, Zukwe aliendelea kutafakari maarifa aliyoyapata kupitia mazungumzo yao. Alidhamiria kuboresha biashara yake ya mbuzi wa nyama na kuongeza mradi wa kilimo cha mbogamboga ili kujiongezea kipato. Kutokana na mazungumzo yale, Zukwe alipata hamasa ya kufanya kazi kwa bidii zaidi.

Maswali

  1. (a) Maneno yapi matano (5) katika kisa ulichokisoma yana makosa ya kimatamshi?
  2. (b) Sahihisha maneno hayo matano (5) kwa kuandika kwa usahihi.
  3. Unafikiri sababu za makosa ya kimatamshi katika maneno uliyoyabainisha katika 1 (a) ni nini?
  4. Nini athari za makosa ya kimatamshi katika mawasiliano?

Shughuli ya 2.1

Sikiliza mazungumzo yaliyorekodiwa katika vyanzo mbalimbali vya TEHAMA, kisha bainisha maneno yenye makosa ya kimatamshi yaliyojitokeza na kuandika maneno hayo kwa usahihi.

Zingatia

Matamshi ni jinsi ya kutamka maneno ya lugha fulani. Matamshi sahihi ni utamkaji wa maneno kwa kuzingatia kanuni za matamshi ya lugha inayohusika. Mzungumzaji akikosea kutamka neno fulani, humfanya msikilizaji ashindwe kabisa kuelewa au aelewe maana tofauti na aliyoikusudia mzungumzaji. Kwa mfano, katika lugha ya Kiswahili mtu akitamka kura badala ya kula atawasilisha maana tofauti na iliyokusudiwa; hivyo, hukwamisha mawasiliano. Katika lugha ya Kiswahili, kuna vipengele vitatu muhimu vinavyozingatiwa katika matamshi. Vipengele hivyo ni lafudhi, kiimbo na mkazo.

Kusimulia habari kwa kuzingatia lafudhi sahihi

Soma kifungu cha habari kuhusu 'Umuhimu wa Michezo', kisha simulia kwa kuzingatia lafudhi sahihi.

Wanafunzi wa kidato cha Kwanza katika shule ya Sekondari Maji Marefu walishiriki mashindano ya UMISSETA. Wavulana walishiriki mashindano ya mpira wa miguu na wasichana walishiriki mpira wa pete. Katika mashindano hayo, timu ya mpira wa miguu ilishinda magoli matatu dhidi ya timu ya Sekondari Nua ambayo ilishinda goli moja. Nayo timu ya mpira wa pete ilibuka kidedea kwa kushinda magoli matano dhidi ya timu ya Shule ya Sekondari Mave ambayo ilishinda kwa magoli mawili. Timu ya mpira wa miguu na timu ya mpira wa pete kutoka Shule ya Sekondari Maji Marefu zilizawadiwa medani na kombe kwa ushindi huo. Baada ya mashindano kuisha, walirudi shuleni ambapo walipokelewa kwa shangwe na vifijo kwani walimu na wanafunzi wenzao walifurahia sana ushindi huo ulioifanya shule yao kuweka historia katika michezo ya UMISSETA kitaifa.

Mwalimu Mkuu aliwashukuru wanafunzi wote walioshiriki katika mashindano hayo. Pia, aliwapongeza na kuwasihi waendelee kufanya mazoezi na kupenda michezo. Aliendelea kusema kuwa michezo ni muhimu kwani huibua vipaji na kuwapatia watu ajira. Hata wachezaji maarufu walianzia chini kama wao. Naye mwalimu wa michezo wa shule hiyo aliwashauri wanafunzi wengine kujiunga na michezo kwani michezo ni afya na inasaidia sana katika kuimarisha mwili na kuwa wakakamavu.

Zingatia

Lafudhi ni namna ya uzungumzaji au usemaji unaoipa utambulisho jamii fulani kutokana na lugha yao ya kwanza. Lafudhi ya mtu huweza pia kutokana na athari za jamii inayomzunguka hata kama jamii hiyo haizungumzi lugha yake ya kwanza. Hivyo, lafudhi hutambulisha jamii au eneo analotoka mzungumzaji kama vile Mara, Kigoma, Rukwa, Mtwara, Singida, Mbeya, Arusha au Pemba.

Shughuli ya 2.2

  1. Sikiliza mazungumzo yenye lafudhi tofauti kutoka katika vyanzo mbalimbali, kisha bainisha vipengele vya lafudhi vinavyoitambulisha jamii husika.
  2. Simulia kisa chochote unachokifahamu kwa kuzingatia lafudhi sahihi ya Kiswahili.

Kusimulia habari kwa kuzingatia kiimbo

Soma simulizi kuhusu 'Kijana Msafiri', kisha isimulie na kujibu maswali yanayofuata.

Kijana msafiri, aitwaye Jumaleo, aliota ameanza safari ya uthubutu. Alifungasha vitu vyake muhimu tayari kwa kuanza safari kutakapopambazuka. Ilipofika majira ya saa kumi na moja alfajiri, giza lilikuwa bado limetanda. Akajisemea moyoni;

"Majira ya alfajiri, anga bado limefunga; je, kuna kitu kinacholizunguka asubuhi hii?"

"Mh! Naona ni asubuhi lakini bado giza; kwa hali hii, inawezekana mvua ikanyesha."

Jumaleo hakuishia hapo. Pamoja na hali iliyokuwa imewamba, aliamua kuanza safari yake. Njiani alikutana na viumbe na mandhari ya kuvutia. Moyo wake ulijawa na mshangao alipokuwa akipita mahali asipopajua na kuona maajabu yake. Ghafla! Aliangukia kwenye pori lenye utulivu! Alionekana kuwa na hofu. "Mh! Kunapitika kweli?" Aliwaza. Punde si punde, sauti ya simba ikasikika. "Lo! ni nani anayewindwa muda huu?" Alisikika Jumaleo akijiuliza. Pamoja na hofu iliyokuwa imetanda, bado hakukata tamaa. Aliendelea na safari yake mpaka ayafikie malengo yake. Njiani alikabiliana na changamoto na vizuizi kwa ujasiri. Alipambana nazo bila woga. Alijiuliza moyoni, "Safari yangu itaishia wapi? Mbona barabara ni ndefu na ngumu?" Hata hivyo, aliendelea na safari akiwa na hamu ya kufika anakoelekea.

Alipokuwa akiendelea na safari, alikutana na pango la ajabu lenye mlango wa dhahabu. Akajisemea moyoni, "Hapahapa ndipo mwisho wa safari yangu." Akaamua kuingia ili apumzike kwa kuwa giza lilikuwa limetanda. Ghafla, alikutana na joka la kutisha kwenye mlango wa pango. Magamba yake yalikuwa yakinemeta mithili ya mwanga wa jua. Kumbe mlango huo ulikuwa ukilindwa na hilo joka! Ama kweli, kukwangua kichwa, hakukunyimi chombo. Kwa ujasiri mkubwa, Jumaleo alikabiliana na lile joka. Baada ya pigano la muda mrefu, Jumaleo aliibuka mshindi; alisikika akisema, "Kweli kufika kwa mguu, hakuhesabu ujanja."

Angali akitafakari jinsi safari yake iliyokuwa na changamoto, ghafla Jumaleo aliamka usingizini na kujiona yuko palepale nyumbani kwake. Hakika ndoto ni kitu cha ajabu sana. Jumaleo alifurahi kuamka kwani ndoto hiyo ilikuwa ya kutisha sana.

Maswali

  1. Ni ujumbe gani unaoupata kutokana na simulizi uliyoisoma?
  2. Unafikiri kwa nini Jumaleo alifurahi baada ya kugundua kuwa safari yake ilikuwa ndoto tu?
  3. Viimbo gani vinajitokeza katika simulizi uliyoisoma?
  4. Kutokana na simulizi uliyoisoma, kuna umuhimu gani wa kutumia viimbo?

Zingatia

Mazungumzo yoyote huwa na lengo mahususi. Ili lengo la mazungumzo liweze kufikiwa kikamilifu, mzungumzaji hana budi kuzingatia kiimbo katika utamkaji wa tungo. Kiimbo huhusu upandaji na ushukaji wa mawimbisauti wakati wa utamkaji. Kila lugha ina utaratibu wake maalumu wa upandaji na ushukaji wa mawimbisauti katika utamkaji wake. Kuna aina nne za kiimbo katika Kiswahili, ambazo ni: kiimbo cha maelezo, kiimbo cha swali, kiimbo cha amri, na kiimbo cha mshangao.

Kiimbo cha maelezo huwa na mawimbisauti yanayoshuka mwishoni mwa tungo. Kiimbo cha swali huwa na mawimbisauti ya kupanda yanapokaribia mwishoni mwa usemi. Kiimbo cha amri huwa na mawimbisauti ya kushuka au kubaki kati wakati wa utamkaji. Kiimbo cha mshangao hujitokeza kwa kupandisha, kushusha, kupandisha na kushusha au kushusha na kupandisha mawimbisauti katika utamkaji kulingana na muktadha wa wazungumzaji.

Mifano:

(i) Amani ameleta matofali. (kiimbo cha maelezo)
(ii) Amani ameleta matofali? (kiimbo cha swali)
(iii) Amani, leta matofali. (kiimbo cha amri)
(iv) Mh! Amani ameleta matofali! (kiimbo cha mshangao)

Kiimbo ni muhimu katika mazungumzo kwa kuwa hubainisha lengo la mzungumzaji kama ni kuuliza swali, kutoa maelezo au ufafanuzi wa kinachozungumzwa, kuvuta usikivu wa msikilizaji, kutoa amri pamoja na kuonesha hisia za mzungumzaji. Vilevile, kiimbo huashiria pumziko kubwa na dogo katika utamkaji wa tungo.

Shughuli ya 2.3

Sikiliza hadithi kutoka vyanzo mbalimbali, kisha isimulie kwa kuzingatia viimbo sahihi.

Kuandika hadithi kwa kuzingatia uhusiano sahihi wa maneno katika sentensi

Soma habari kuhusu 'Bidii ya Faji', kisha jibu maswali yanayofuata.

Mwalimu Utete alipomaliza kufundisha Somo la Kiswahili alitoa zoezi na kumtaka kila mwanafunzi akajifunza namna maneno yanavyopangiliwa na kuhusiana katika kujenga sentensi zenye maana. Faji alikuwa mwanafunzi mmojawapo katika darasa hilo. Faji alikuwa na bidii sana katika kujifunza na alihakikisha kila wakati anaveka juhudi katika masomo yake.

Kila siku baada ya saa za shule, Faji alikuwa na kawaida ya kwenda kwa shangazi yake, aliyeitwa Juhudi, ambaye alikuwa mfugaji na mtaalamu wa lugha. Siku hiyo Faji alipokuwa akioka shuleni, alikumbuka kuwa shangazi yake ni mtaalamu wa lugha. Alijisemea moyoni, "Nikitika tu nitamwomba shangazi anifundishe namna maneno yanavyopangiliwa na kuhusiana katika kujenga sentensi." Baada ya Faji kufika kwa shangazi yake, alimsalimu na kumuuliza, "Shangazi, ni kwa namna gani maneno huhusiana na kufuatana mpaka tunakuwa na sentensi zenye maana?"

Juhudi alitabasamu na kumwambia, "Kabla ya kujua uhusiano, ni maneno gani unayoyafamu?" Faji alimjibu shangazi yake kwa kusema, "Shangazi, ninajua maneno yanayotaja majina ya watu na mimea, maneno yanayotoa taarifa kuhusu majina, maneno yanayoeleza namna tendo lilivyofanyika na maneno yanayoeleza mahali tendo lilipofanyikia." "Vizuri sana Faji," Juhudi alijibu. "Kwanza, unatakiwa ujue kuwa maneno yote tunayotumia yamegawanyika katika makundi. Ninamba usikilize kwa makini maelezo yangu. Kutokana na ufafanuzi nitakaoutoa nina hakika utaweza kueleza uhusiano uliopo baina ya maneno hayo nitakayoyazungumzia."

Juhudi alianza kwa kumweleza Faji kuhusu aina za maneno zilizopo katika lugha ya Kiswahili. Alizitaja aina hizo kuwa ni: Nomino (N), Kiwakilishi (W), Kivumishi (V), Kitenzi (T), Kielezi (E), Kiunganishi (U), Kihusishi (H) na Kihisishi (Hs).

Juhudi hakuishia hapo, aliendelea kwa kusema kuwa, katika aina hizo, ziko baadhi ya aina za maneno ambazo zimegawanyika zaidi ndani yake kutokana na dhima ya kila aina. Juhudi alianza kumweleza Faji kuhusu nomino. Alimwambia kuwa nomino ina kazi ya kutaja majina ya watu, vitu, mahali na hali. Aliendelea kufafanua kuwa nomino imegawanyika katika makundi manne ambayo ni: nomino za pekee, kawaida, dhahania na jumla.

Juhudi alitaja aina nyingine ya maneno kuwa ni viwakilishi. Alisema, maneno haya ni mbadala wa nomino katika sentensi. Viwakilishi vimegawanyika katika makundi matano ambayo ni nafsi, idadi, viulizi, vimilikishi, sifa na vioneshi.

Aidha, aliendelea kumfafanulia Faji aina nyingine ya maneno ambayo ni vivumishi. Alifafanua kuwa maneno haya yana kazi ya kusifia au kutoa taarifa zaidi kuhusu nomino na viwakilishi. Maneno haya yamegawanyika katika makundi mbalimbali, ambayo ni: vivumishi vya sifa, idadi, viulizi, a-unganifu, vimilikishi, pekee na vioneshi. Aliendelea kusema kuwa, ikiwa kivumishi kitatokea sehemu ambayo hapana nomino wala kiwakilishi, sifa yake ya kuvumisha itapotea; hivyo, kitabeba sifa nyingine.

Vilevile, Juhudi alifafanua aina nyingine ambayo ni vitenzi. Alisema maneno haya hueleza tendo lililofanyika, linalofanyika au litakalofanyika. Aina hii imegawanyika katika makundi matatu, ambayo ni: kitenzi kikuu (T) ambacho kwa hakika huarifu tendo kuu katika sentensi. Aidha, aliendelea kutoa ufafanuzi wa kitenzi kisaidizi (Ts). Alisema kwamba kitenzi kisaidizi hufanya kazi ya kusaidia kitenzi kikuu kukamilisha taarifa katika sentensi. Vilevile, alifafanua kuhusu kitenzi kishirikishi (t) ambacho hufanya kazi ya kushirikisha vitu mbalimbali kihali, kitabia au kimazingira.

Faji alikuwa na hamu zaidi ya kujifunza na aliendelea kusikiliza kwa makini. Juhudi alimweleza kuhusu vielezi kuwa ni maneno yanayotoa taarifa zaidi kuhusu kitenzi, kivumishi au kielezi chenyewe. Aliendelea kusema kuwa vielezi vimegawanyika katika makundi manne ambayo ni mahali, wakati, namna na idadi.

Zaidi ya hayo, Juhudi alimweleza kuhusu viunganishi kwa kusema kuwa haya ni maneno ambayo huunganisha maneno au vifungu vya maneno. Pia, alifafanua kuhusu vihusishi kuwa ni maneno yenye dhima ya kuhusisha maneno katika tungo. Kadhalika, alimweleza kuhusu vihisishi kwa kusema kuwa ni maneno yanayoonesha hisia za mzungumzaji. Baada ya ufafanuzi huo Juhudi aliandaa kielelezo ambacho kilimsaidia Faji kuelewa aina za maneno.

Aina za Maneno katika Kiswahili

1. Nomino (N)

Maneno yanayotaja majina ya watu, vitu, mahali na hali.

Aina ndogo: pekee, kawaida, dhahania, jumla

Mifano: Juma, nyumba, hasira, jeshi

2. Kiwakilishi (W)

Maneno yanayofanya kazi badala ya nomino.

Aina ndogo: nafsi, idadi, viulizi, vimilikishi, vioneshi, sifa

Mifano: mimi, wawili, nani, wangu, huyo, mrefu

3. Kivumishi (V)

Maneno yanayosifia au kutoa taarifa zaidi kuhusu nomino na viwakilishi.

Aina ndogo: sifa, idadi, viulizi, vioneshi, vimilikishi, pekee

Mifano: baya, tatu, ngapi, huyo, yangu, Kilimanjaro

4. Kitenzi (T)

Maneno yanayoeleza tendo lililofanyika, linalofanyika au litakalofanyika.

Aina ndogo: kikuu, kisaidizi, kishirikishi

Mifano: anacheka, aliweza, ni

5. Kielezi (E)

Maneno yanayotoa taarifa zaidi kuhusu kitenzi, kivumishi au kielezi chenyewe.

Aina ndogo: mahali, wakati, namna, idadi

Mifano: shuleni, leo, vizuri, mara mbili

6. Kiunganishi (U)

Maneno yanayounganisha maneno au vifungu vya maneno.

Mifano: na, lakini, au

7. Kihusishi (H)

Maneno yenye dhima ya kuhusisha maneno katika tungo.

Mifano: katika, kwa, kwenye

8. Kihisishi (Hs)

Maneno yanayoonesha hisia za mzungumzaji.

Mifano: lo!, aisee!, du!

Maswali

  1. Habari uliyoisoma inazungumzia nini?
  2. Aina zipi za maneno zimezungumziwa katika habari uliyoisoma?
  3. Kutokana na habari uliyoisoma, maneno gani hufanya taarifa ya sentensi ikamilike?
  4. Ni maneno yapi yanayodokeza sifa za nomino au viwakilishi?
  5. Vielezi vina umuhimu gani katika sentensi?

Zingatia

Lugha ya Kiswahili ina aina nane (8) za maneno. Baadhi ya aina hizo za maneno zina aina ndogondogo ndani yake. Aina ya kwanza ni nomino, ambayo ina nomino za pekee, za kawaida, dhahania na za jumla. Nomino za pekee ni majina ya watu au maneno mahususi ambazo huanza kwa herufi kubwa zinapoandikwa kama vile Juma, Dodoma na Kilimanjaro; nomino za kawaida ni majina ya vitu mbalimbali visivyo vya pekee kama vile nyumba, mit na gari; nomino dhahania ni zile zinazotaja vitu visivyoonekana wala kushikika kama vile usingizi, hasira na ndoto; na nomino za jumla ni zile zinazotaja vitu katika kundi kama vile jeshi, timu na tume.

Vilevile, viwakilishi navyo viko vya aina tano: viwakilishi vya nafsi kama vile mimi, wewe, sisi, na yeye; viwakilishi vya idadi kama mmoja, wawili, na watano; viwakilishi viulizi kama vile nani, wapi, yupi, na nini; viwakilishi vimilikishi kama vile wangu, langu, na chetu; viwakilishi vioneshi kama vile huyo, huyu, na wale; na viwakilishi vya sifa kama vile mrefu, mnene na mweusi.

Kadhalika, vivumishi viko vya aina mbalimbali. Miongoni mwa aina hizo ni: vivumishi vya sifa kama vile baya, jeupe, na zuri; vivumishi vya idadi kama vile tatu, chache, na nyingi; vivumishi viulizi kama vile ngapi, yupi, na nani; vivumishi vioneshi kama vile huyo, yule, na hicho; na vivumishi vimilikishi kama vile yangu, vyetu, na yake. Wakati mwingine jina pia huweza kuvumisha jina lingene kama vile katika mlima Kilimanjaro, Mwalimu Ana na Katibu Kata.

Vitenzi navyo vimegawanyika katika aina tatu ambazo ni vitenzi vikuu kama vile anacheka, anasoma, na anapika; vitenzi visaidizi kama vile alikawa, aliweza, na huwa (hasa vinapotumika na vitenzi vikuu); na vitenzi wishirikishi kama vile si, ni, na ndiye.

Pia, vielezi vimegawanyika katika aina nne ambazo ni: vielezi vya mahali kama vile juu ya, chini ya, na shuleni; vielezi vya wakati kama vile mwaka jana, leo, na asubuhi; vielezi vya namna kama vile vizuri, harakaharaka, na polepole; na vielezi vya idadi au kiasi kama vile mara mbili, mara chache, na mwaka mmoja.

Zoezi la 2.2

  1. Chunguza sentensi zifuatazo, kisha bainisha aina za maneno yaliyounda sentensi hizo.
    1. Jengo refu limebomoka leo.
    2. Mwanafunzi yule anaandika kwa kalamu.
    3. Maembe na machungwa yamekomaa.
    4. Yule amekwenda shuleni kwa miguu.
    5. Lo! Mwanafunzi nadhifu amefaulu mtihani.
    6. Mimi ninapenda kujifunza Kiswahili.
    7. Kokoto zile zimekusanywa na wanakijiji.
    8. Wawili wameondoka juzi.
    9. Wale watacheza mpira kesho.
  2. Tunga sentensi mbili kwa kila aina ya kiwakilishi.
  3. Tunga sentensi mbili kwa kila aina ya kivumishi.

Shughuli ya 2.5

Andika hadithi kuhusu shujaa mmojawapo unayempenda kwa kuzingatia uhusiano sahihi wa maneno katika sentensi.

Zoezi la Marudio la 2

1. Jibu maswali yafuatayo kwa kuandika herufi ya jibu sahihi.

  1. Kumbo na Kapelo walikuwa wanabishana kuhusu muundo wa sentensi. "Mimi nitafua na wewe utaosha vyombo." Upi ni muundo sahihi wa sentensi hiyo?
    1. E T U W T N
    2. W T U W T E
    3. W T U W T N
    4. V T U W T E
    5. N T U W T N
  2. Ipi si dhima mojawapo ya kiimbo kati ya hizi zifuatazo?
    1. Kubadili maana ya neno
    2. Kuuliza swali
    3. Kusisitiza jambo
    4. Kuonesha hisia
    5. Kubadili maana ya tungo
  3. "Mama alinunua vyombo vizuri. Vizuri vyote vilivekwa kabatini. Mimi niliyipanga vizuri." Katika mfuatano wa sentensi hizo, neno vizuri limetumikaje?
    1. Kiwakilishi, kivumishi, kielezi
    2. Kivumishi, kielezi, kiwakilishi
    3. Kielezi, kivumishi, kiwakilishi
    4. Kiwakilishi, kielezi, kivumishi
    5. Kivumishi, kiwakilishi, kielezi
  4. Sentensi ipi kati ya hizi zifuatazo ina makosa ya kimatamshi?
    1. Kaka amerūa nguo.
    2. Osha sahani uliyolia chakula.
    3. Suedi amenunua mbuzi.
    4. Eva amenunua kanga.
    5. Joni amempigia npila Asha.
  5. Upi si umuhimu wa kuzingatia ushikamani wa sentensi katika aya?
    1. Kuleta maana ya sentensi katika aya
    2. Kufanya aya iwe ndefu
    3. Kuleta uhusiano wa kimaana
    4. Kuonesha ushikamani wa kimawazo
    5. Kuleta mitiririko wa mawazo

2. Oanisha sentensi zenye matumizi ya vivumishi katika Orodha A na aina ya kivumishi husika kutoka Orodha B kwa kuandika herufi ya jibu sahihi.

Orodha A Orodha B
(i) Mwalimu wetu alileta kitabu darasani. A. Kivumishi cha jina
(ii) Wanafunzi wale wanafanya mazoezi uwanjani. B. Kivumishi kiulizi
(iii) Mjomba Kichau amesafiri. C. Kivumishi cha idadi
(iv) Wanakijiji wangapi wamepiga kura? D. Kivumishi cha sifa
(v) Watoto watatu wamesimuliwa hadithi. E. Kivumishi cha pekee
(vi) Askari hodari amemkamata mwizi. F. Kivumishi kimilikishi
G. Kivumishi kioneshi
H. Kivumishi cha taarifa

3. Bainisha maneno yenye makosa ya kimatamshi katika sentensi zifuatazo kwa kuyapigia mstari, kisha andika sentensi hizo kwa usahihi.

  1. Mwanafunzi anayejitambua hapendagi mzaha katika masomo.
  2. Shule yetu ina vifaa vya samani.
  3. Mit ulokuwa kalibu na bustani ya maua umeanguka.
  4. Mzee Kiza amedhuru mbuga za wanyama.

4. Tunga sentensi zenye miundo ifuatayo:

  1. N T N E
  2. N V T N V
  3. W Ts T N
  4. N t N
  5. Hs T E
  6. N U N T
  7. N T H N

5. Matumizi ya kiimbo husaidia kubainisha lengo la mzungumzaji. Fafanua malengo ya mzungumzaji katika sentensi zifuatazo:

  1. Mwanafunzi anasoma kwa bidii.
  2. Mwanafunzi, soma kwa bidii.
  3. Mwanafunzi anasoma kwa bidii?
  4. Mwanafunzi anasoma kwa bidii!

6. Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia maneno uliyopewa katika kisanduku.

gari, mwema, wao, shambani, ili, aisee, katika, si, pikipiki, kwa sababu

  1. Mwanafunzi anatakiwa kusoma vitabu vingi ……… kupata maarifa.
  2. ……… lake limeharibika.
  3. Mtoto ……… huwabeshimu watu wote.
  4. ……… wamemaliza kazi yao kwa wakati.
  5. Mkulima amepanda mazao mengi ……….
  6. ………! Kijana huyo anajituma sana.
  7. Maki ……… mtundu.
  8. Babu anapenda kupumzika ……… bustani ya maua.
Sura ya Tatu: Matumizi ya Kamusi

Sura ya Tatu: MATUMIZI YA KAMUSI

Utangulizi

Maana za maneno hutegemeana na muktadha wa matumizi. Watumiaji wa lugha wanapaswa kujua matumizi sahihi ya maneno ili waweze kuwasiliana kwa ufasaha. Katika sura hii utajifunza kutumia kwa usahihi msamiati na taarifa mbalimbali za kamusi katika mazungumzo na maandishi.

Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuelewa maana na matumizi ya maneno mbalimbali kwa usahihi. Vilevile, utakusaidia kuelewa namna ya kutumia kamusi.

Fikiri: Kujifunza lugha bila kutumia kamusi

Kutumia msamiati kwa usahihi

Soma habari kuhusu 'Yaliyosahaulika' kisha jibu maswali yanayofuata.

Mzee Masika aliishi katika mji mdogo uitwao Amani. Masika alikuwa mtu mwenye furaha na tabasamu wakati wote. Mara nyingi Masika alijitahidi kukumbuka matukio muhimu ya maisha yake ya zamani. Masika alikuwa na mjukuu wake aitwaye Furaha. Masika alikuwa na kawaida ya kutembelea bustani yake kila siku. Siku moja, wakati wa mchana, jua lilikuwa likiwaka sana, akaamua kwenda kutembelea bustani yake.

Akiwa bustanini, jambo lisilo la kawaida lilitokea. Msichana mdogo alimkaribia kwa tabasamu lenye furaha, akisema kwamba alikuwa mjukuu wake aitwaye Furaha. Mh! Furaha? Ndiye nani? Masika aliuliza. Furaha aligundua kuwa babu yake ameanza kupoteza kumbukumbu. Alimkumbusha babu yake kwa kumsimulia matukio yao alipokuwa mtoto. Ghafla! Machozi yalijaa machoni mwa Masika alipogundua kuwa kweli alikuwa amesahau kama ana mjukuu anayeitwa Furaha.

Furaha alipoona hali hiyo, aliamua kushinda na babu yake siku nzima bustanini. Furaha aliendelea kumsimulia matukio mbalimbali. Kwa kila tukio, mwanga wa kumbukumbu ulizuka machoni pa Masika. Jua lilipozama, Furaha na Masika walirudi nyumbani. Masika alimshukuru mjukuu wake kwa kumpa siku ya kukumbuka yaliyosahaulika.

Maswali

  1. Nani alikuwa mtu wa furaha na tabasamu katika habari uliyoisoma?
  2. Nini maana za maneno yaliyokozwa wino katika habari uliyoisoma?
  3. Furaha aligundua kuwa babu yake ameanza kufanya nini?
  4. Ni funzo gani ulilolipata kutokana na habari uliyoisoma?
  5. Nini tofauti ya maneno yafuatayo?
    1. tabasamu na cheka
    2. mchana na kutwa
    3. kumbukumbu na kumbuka

Zingatia

Kamusi ni kitabu cha rejea chenye orodha ya maneno na ufafanuzi wake yaliyopangwa kwa utaratibu maalumu wa alfabeti (A – Z). Maneno hayo hukusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa lugha inayotungiwa kamusi na kutolewa ufafanuzi wa maana zake kwa lugha hiyo yenyewe au kwa lugha nyingine. Kwa kawaida, maneno hufafanuliwa kwa namna ambayo msomaji huweza kuelewa. Hata hivyo, ufafanuzi wa maneno kwenye kamusi hutegemea lengo la kamusi inayohusika.

Kuna aina mbalimbali za kamusi. Kuna kamusi ya lugha moja, yaani orodha ya maneno pamoja na maelezo yake yanakuwa katika lugha moja. Vilevile, kuna kamusi ya lugha mbili au zaidi, kwa maana ya neno kuwa lugha fulani na kufafanuliwa kwa maelezo ya lugha nyingine. Aidha, kamusi inaweza kuwa ya somo mahususi au uwanja fulani kama vile methali, vitendawili, nahau na visave.

Shughuli ya 3.1

Chunguza Kielelezo Na. 3.1, kisha fanya yafuatayo:

  1. Bainisha maneno matano (5) yaliyokozwa wino, kisha andika maana zake kutokana na Kielelezo Na. 3.1.
  2. Eleza kwa nini maneno yaliyokozwa wino katika ukurasa wa kamusi yameanza na herufi zinazofanana.
  3. Toa ufafanuzi kuhusu utaratibu uliotumika kuandika maneno yaliyokozwa wino katika kielelezo hicho.

Muundo wa Kamusi

Mfano wa Ukurasa wa Kamusi

bumbuazi /bumbu'azi/ nm (t) [k/z+] hali ya kuwa kimya na kutojua la kufanya au kutosikia lisemwalo tara butaa, butwaa, mshangao: Pigwa na ~; Shikwa na ~.

bumbura /bumbura/ nm (t) [a/wa-] samaki wa maji chumvi mwenye macho manene anayefanana na chewa au mzia lakini mfupi.

bumburuk.a /bumburuka/ kt [sic] (~la, ~ika, ~isha) 1 shtuka ghafla na kwenda mbio k.v. kundi la ndege au wanyama wanapokurupushwa tara kurupuka. 2 amka kwa kisho, 3 julikana au fichuka: Siri ime~.

bumla /bu'mia/ nm (t) [k/z+] (kb) kipande cha ubao kilichomo jahazini kinachofungwa kwenye mkuku na kubeba fashini. (>Kaj)

bunduki /bu'nduki/ nm (t) [k/z+] silaha ya kuliwatulia risasi kwa nguvu tara mrau¹. (>Kar/Khi)

Sehemu za Kamusi

1. Kidahizo (neno kuu)

Haya ni maneno yanayoorodheshwa kwenye kamusi kwa chapa iliyokozwa au kwa kuwekwa rangi kwa lengo la kutofautishwa na maneno mengine.

2. Matamshi

Huoneshwa kwa kutumia alama za mabano ya mshazari (/ /).

Mifano: lima /'lima/, hadimu /ha`dimu/, kikapu /ki`kapu/

3. Aina ya neno

Hubainishwa kwa kifupisho (k.m. nm = nomino, kt = kitenzi, kv = kivumishi, n.k.)

4. Ngeli

Huoneshwa kwenye mabano (k.m. (t), (ma), (ki), n.k.)

5. Ufafanuzi wa maana

Hutoa maelezo ya kina kuhusu maana ya neno.

6. Mifano ya matumizi

Huoneshwa kwa kutumia herufi italiki au alama maalumu.

Zingatia

Maneno yote yanayoingizwa katika kamusi hupangwa kwa utaratibu wa alfabeti. Maneno yanayoanza na herufi a, huwekwa chini ya herufi A. Vivyo hivyo, kwa maneno yanayoanza na herufi b, ch, d hadi z. Ikiwa herufi za kwanza za maneno zinafanana, basi inaangaliwa herufi ya pili, tatu na kuendelea mpaka lipatikane neno linalostahili kuanza.

Kwa mfano, maneno kaka, keki, kiko, koti na kuti. Maneno yote haya yanaanza na herufi k. Hivyo, imeangaliwa herufi ya pili ambayo ndiyo imeongoza kuyapanga maneno, yaani kwa kufuata irabu a, e, i, o na u. Kama herufi za pili zingefanana kwa maneno yote, tungeangalia herufi ya tatu na kuendelea mpaka maneno yote yapangwe kwa usahihi.

Kidahizo ndilo neno kuu katika kamusi. Haya ni maneno yanayoorodheshwa kwenye kamusi kwa chapa iliyokozwa au kwa kuwekwa rangi kwa lengo la kutofautishwa na maneno mengine. Kidahizo pamoja na maelezo yake kwa pamoja huitwa kitomeo. Ikiwa neno lina maana zaidi ya moja, maana zote huorodheshwa kwa kupewa namba. Mtumiaji wa kamusi anapaswa kuzisoma na kuona ni ipi inaendana na kile anachokitafutia maana kwa kuhusisha mazingira ambamo neno linalohusika limetumika.

Kutumia taarifa za kamusi katika mawasiliano

Soma shairi lifuatalo la 'Ndege wangu nampenda', kisha jibu maswali yanayofuata.

Mhariri mchapaji, niweke japo pembeni,

Niwaeleze walaji, walao ndege porini,

Ndege wangu mjuaji, mgumu hapatikani,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Ndege nahangaikia, huku na kule porini,

Naye kanidengulia, nikawa nipo tabuni,

Wengi nikawatumia, mafanikio sioni,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Wa kwanza nikamtuma, jinale ndiye Mwazani,

Amshike kwa mtama, hata kama mtegoni,

Mwazani akachtutama, hakumtia kapuni,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Domitila ni wa pili, nikamweleza yakini,

Fanya kila hila hali, nimtie mikonomi,

Ndege japo ni mkali, tamtuliza tunduni,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Afiswa ndiye wa tatu, nitamweleza yakini,

Katika ndege watatu, mmoja namtamani,

Usimlete kifutu, ambaye simtamani,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Afiswa katekeleza, akamtega mini,

Na mtama wa kumeza, ndege akautamani,

Akajaa kama pweza, anavyojaa wavuni,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Ndege nikakabidhiwa, nikamtia tunduni,

Sitaki akatolewa, na mwingine asilani,

Na jina akatungiwa, MAGNET la utani,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Siku napata safari, ya kwenda zangu mjini,

Nanunua vya fahari, ndege awe furahani,

Fulana na vya hariri, kitambaa na kidani,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Tama hapa nimefika, ndege yuko furahani,

Hakuna wa kumshika, na sasa yupo nyumbani,

Chumbani arukaruka, hajali wala haoni,

Nampenda ndege wangu, sababu kanipa tabu.

Chanzo: Gazeti la Uhuru, Aprili 12, 1991

Maswali

  1. Shairi ulilolighani linahusu nini?
  2. Nini maana za maneno yafuatayo kulingana na yalivyotumika katika shairi ulilolighani? Tumia kamusi kupata maana hizo.
    1. dengulia
    2. chutama
    3. hila
    4. fahari
    5. hariri
    6. kidani
  3. Maneno yaliyokozwa wino katika kamusi yanaitwaje?

Zoezi la 3.1

  1. Bainisha aina mbalimbali za kamusi za Kiswahili unazozijua.
  2. Bainisha vipengele vitatu vinavyopatikana katika kamusi.
  3. Tumia maneno yafuatayo kutunga sentensi kulingana na maana za maneno hayo katika kamusi.
    1. mgogoro
    2. kanyaga
    3. gawa
    4. chujio
    5. sabahi

Zingatia

Kamusi ina dhima mbalimbali. Dhima mojawapo ni kudokeza taarifa mbalimbali za kisarufi kama vile aina za maneno (nomino, vitenzi, vielezi, vivumishi, viwakilishi, viunganishi, vihusishi na vihisishi) na ngeli za nomino ambazo hujipambanua katika umbo la umoja na wingi. Aghalabu, vidahizo huandikwa kwa umoja na wingi na huoneshwa kwenye mabano.

Vilevile, kamusi huonesha mifano ya matumizi ya methali, misemo na nahau; kwa mfano, ~ na ~ hujaza kibaba (methali). Methali hii hutumiwa kuonesha matumizi ya neno moja ambalo nafasi yake huoneshwa kwa alama ya wimbi (~). Mathalani, katika mfano wa methali uliobainishwa hapo juu, alama ya wimbi imetumika kuwakilisha neno haba. Mbali na kuonesha mifano ya matumizi ya maneno, kamusi hutumika kuonesha mnyambuliko wa vitenzi. Baada ya maelezo ya maana, mnyambuliko wa kitenzi hubainishwa kwa kutumia alama ya wimbi ikifuatiwa na viambishi nyambulishi; kwa mfano, Fumbu.a /fumbua/ kt [ele] 1 eleza siri au habari au jambo lilo gumu kufahamika; 2 funua ili kuwa wazi: ~ana, ~ka, ~lia, ~liana, ~lisha, ~liwa.

Kadhalika, kamusi hutumika pia kuonesha matamshi ya maneno ya lugha iliyoandikiwa. Matamshi haya huoneshwa kwa kutumia alama za mabano ya mshazari (/ /).

Kupitia taarifa za matamshi, kamusi humsaidia mtumiaji kujua namna ya kutamka maneno anayoyatafuta katika kamusi. Kamusi za Kiswahili zipo za aina mbalimbali kama vile kamusi za lugha moja, kamusi za lugha mbili au lugha tatu. Pia, zipo kamusi za masomo au fani mahususi kama vile kamusi ya fasihi, kamusi ya visawe, kamusi ya misemo, kamusi ya tiba, na kadhalika.

Aina za Kamusi

Jamii Mbalimbali za Kamusi

1. Kamusi ya Lugha Moja

Kamusi ambayo maneno na ufafanuzi wake yote yamo katika lugha moja.

Mfano: Kamusi ya Kiswahili Sanifu

2. Kamusi ya Lugha Mbili

Kamusi ambayo inatafsiri maneno kutoka lugha moja hadi nyingine.

Mifano: Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza, Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili

3. Kamusi ya Fani Maalumu

Kamusi inayojikita katika istilahi za uwanja maalumu.

Mifano: Kamusi ya Tiba, Kamusi ya Sayansi, Kamusi ya Fedha

4. Kamusi ya Visawe

Kamusi inayoorodhesha maneno yenye maana zinazofanana.

Mfano: Kamusi ya Visawe vya Kiswahili

5. Kamusi ya Misemo na Methali

Kamusi inayojikita katika misemo, methali na vitendawili.

6. Kamusi ya Kielelezo

Kamusi inayotumia picha na michoro kufafanua maana za maneno.

Vipengele Muhimu vya Kamusi

  1. Utangulizi/Mwongozo - Maelekezo ya jinsi ya kutumia kamusi
  2. Orodha ya Alfabeti - Ratiba ya herufi kwa utaratibu
  3. Vidahizo - Maneno yaliyoorodheshwa kwa utaratibu wa alfabeti
  4. Ufafanuzi wa Maana - Maelezo ya kina ya maana za maneno
  5. Mifano ya Matumizi - Vifungu vya maneno vinavyoonesha matumizi ya maneno katika muktadha
  6. Vifupisho na Alama - Mfumo wa kueleweshana kati ya mtumiaji na kamusi
  7. Nyongeza - Sehemu za ziada kama vile orodha ya nchi, ramani, n.k.

Zoezi la Marudio la 3

1. Kama maneno katika kamusi yatapangwa bila kufuata mpangilio maalumu, ni changamoto gani zinaweza kujitokeza?

2. Eleza maana za maneno yafuatayo kwa kutumia kamusi, kisha tunga sentensi moja moja kwa kutumia maneno hayo.

  1. utandawazi
  2. buli
  3. figa
  4. dalali
  5. pika
  6. kakakaka
  7. mtaalamu
  8. pambana
  9. rushwa
  10. sera

3. Bainisha mambo ya kuzingatia wakati wa kutafuta maana za maneno katika kamusi.

4. Orodhesha kialfabeti maneno yaliyomo katika kisanduku, kisha tumia kamusi kuonesha mkazo wa maneno hayo.

mdau, mfalme, ua, elimu, usalama, taifa, baba, kula, safari, familia

Shughuli ya Ziada

Tembelea maktaba ya shule yako au maktaba ya jamii na uchunguze kamusi tofauti tofauti. Andika orodha ya aina tano za kamusi ulizozikuta na ueleze kwa ufupi tofauti zake.

Mbinu za Kutumia Kamusi Kwa Ufanisi

Hatua za Kutumia Kamusi

  1. Tambua neno unalotaka kufahamu - Hakikisha unajua herufi za kwanza za neno hilo.
  2. Fuata utaratibu wa alfabeti - Tafuta sehemu ya kamusi inayohusiana na herufi ya kwanza ya neno lako.
  3. Angalia herufi za pili na za mfululizo - Endelea kutafuta kwa kuzingatia herufi za pili, tatu na kadhalika.
  4. Soma ufafanuzi wote - Kama neno lina maana zaidi ya moja, soma zote na uchague inayofaa zaidi kwa muktadha wako.
  5. Angalia mifano ya matumizi - Hii itakusaidia kuelewa vizuri jinsi neno linavyotumika katika sentensi.
  6. Zingatia taarifa za ziada - Kama matamshi, ngeli, aina ya neno, n.k.

Ushauri wa Kutatua Changamoto

Iwapo hupati neno unalotafuta:

  • Hakikisha umepanga kwa usahihi kufuata alfabeti
  • Angalia uandishi wa neno - labda limeandikwa kwa namna tofauti
  • Tumia kamusi ya kisasa - maneno mapya huongezeka kila wakati
  • Waulize walimu au wataalamu wa lugha
  • Tumia vyanzo vya mtandaoni vinavyokubalika
Sura ya Nne: Kusikiliza Mazungumzo

Sura ya Nne: Kusikiliza Mazungumzo

Utangulizi

Msikilizaji huelewa vizuri mazungumzo kutokana na kusikiliza kwa makini. Katika sura hii, utajifunza kusikiliza mazungumzo changamani, kueleza kwa muhtasari mazungumzo uliyoyasikiliza na kushiriki katika majadiliano ya masuala mbalimbali kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.

Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kujifunza maarifa mapya na kukuza ufahamu. Vilevile, utakuza uwezo wa kueleza masuala mbalimbali kutokana na stadi ya kusikiliza.

Fikiri: Mambo ya kuzingatia katika kusikiliza mazungumzo

Kusikiliza mazungumzo changamani

Sikiliza mazungumzo yafuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Tana:
Unakumbuka jana mwalimu alitufundisha kuhusu nini?
Daba:
Ndiyo. Alitufundisha kuhusu ujasiriamali.
Tana:
Wewe ulichagua kazi gani za mikono kati ya kazi zilizobainishwa?
Daba:
Mimi sikuchagua kazi za mikono bali nilichagua sanaa za maonesho.
Tana:
Kwa nini ulichagua kazi hiyo?
Daba:
Kama unakumbuka, siku aliyokuja mwalimu wa Chuo cha Ufundi Stadi alitueleza kuwa kazi za sanaa zina faida kubwa tukiwa shuleni na hata baada ya kumaliza masomo.
Tana:
Hivi unaielewa vizuri kazi hiyo?
Daba:
Ndiyo. Ni kazi ninayoipenda na inapendwa na watu wengi bara na visiwani. Pia, ni kazi inayowapatia wasanii wengi umarufu ndani na nje ya Afrika.
Tana:
Ha! Ha! Ha! Jambo kubwa kuliko yote umelisahau.
Daba:
Ninalikumbuka Tana, kujipatia ajira. Si lazima tukimaliza kusoma tusubiri serikali itupatie ajira bali tunaweza kujiajiri kwa kutumia ujuzi tulionao. Kufanya hivyo kutaisaidia serikali yetu kupunguza tatizo la watu kukosa ajira.
Tana:
Sawa! Mimi sipendi sanaa za maonesho bali ninapenda sana kazi ya ualimu, kwani nikiwa mwalimu nitawafundisha watu na kuwapatia ujuzi na maarifa.
Daba:
Hee! Tana, kazi ya ualimu utaiweza? Kazi ya ualimu inataka uwe mtu wa kujisomea kila wakati ili uweze kuwapatia wanafunzi maarifa yanayoenda na wakati.
Tana:
Nitaweza Daba. Hiyo ndiyo kazi ninayoipenda sana. Mwalimu wetu wa Kiswahili huwa anatufundisha vizuri sana. Ndiyo maana ninapenda kufundisha.
Daba:
Je, una uhakika wa kuipata ajira ya ualimu? Mimi nimechagua sanaa za maonesho kwani ninajua nitajiajiri mwenyewe hapo baadaye. Wewe je?
Tana:
Mimi ninaipenda kazi ya ualimu. Kumbuka kuwa bila mwalimu huwezi kuipata taaluma ya sanaa za maonesho. Hivyo, ualimu ni kazi muhimu. Hata nisipoajiriwa ninaweza kujiajiri pia.
Daba:
Tana nimekuelewa vizuri. Kazi uliyoichagua ni kazi ya muhimu sana katika ulimwengu tunaoishi. Kwa kuwa wewe unapenda sana kujisomea utakuwa mwalimu bora. Ninashukuru sana kwani umeweza kunieleza umuhimu wa mwalimu.
Tana:
Nami ninakushukuru sana Daba kwani tumeweza kueleweshana mambo mazuri.

Maswali

  1. Unaelewa nini kuhusu dhana ya sanaa za maonesho?
  2. Kutokana na mazungumzo uliyoyasikiliza, Daba alisema ujuzi wa sanaa za maonesho una faida gani kwake?
  3. Unapendelea kufanya kazi gani hapo baadaye? Kwa nini?
  4. Ungepewa nafasi ya kushauri ungewashauri nini wenzako wanaotegemea kuajiriwa ili wapate kipato?
  5. Kwa nini Tana anapenda kufanya kazi ya ualimu?

Shughuli ya 4.1

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, sikiliza mazungumzo changamani, kisha eleza ujumbe ulioupata.

Sifa za lugha ya mazungumzo

Sikiliza kwa makini ngonjera inayotambwa kuhusu "Rushwa", kisha jibu maswali yanayofuata:

Juma:

Rafiki nakueleza, rushwa ni mit mkavu,

Jana nilipokamatwa, kidogo niwekwe ndani,

Nikawaza kuwazua, napaswa nifanye nini?

Ndipo mawazo yakaja, kuuzunguka mbuyu.

Amani:

Rafiki unanikwaza, nyuma 'naturalisheni,

Twatangaza uzalendo, kuacha ya uhaini,

Rushwa adui wa haki, kamwe usiendekeze,

Ukifuata sheria, mambo yatawa murua.

Juma:

Ni kweli uyasemayo, lakini yatulazimu,

Kuweza kujinusuru, vema unyoshe mkono,

Mambo huwa ni magumu, wakubwa wakutabana,

Ndiyo maana ni muhimu, kuwapa ili yaishe.

Amani:

Kamwe sitakushauri, mbuyu kuuzunguka,

Ungeilipa kwa haki, mapato ya serikali,

Miundombinu 'ngejengwa, sote tungenufaika,

Kuliko kunufaisha, yeye aliye mmoja.

Juma:

Macho umenifumbua, ujinga umeni toka,

Jamaa kanifaidi, pesa yangu amekula,

Barabara bado mbovu, 'twarzipita kwa taabu,

Sitatoa tena rushwa, mmoja kunufaisha.

Wote:

Tuungane kwa pamoja, sauti yetu kupaza,

Rushwa hukiuka haki, maendeleo kukwama,

Wachache wanufaika, taifa kutokusonga,

Tukiitokomeza rushwa, uchumi tutainua.

Maswali

  1. Funzo gani uliiolipata kutokana na ngonjera uliyoisikiliza?
  2. Mzungumzaji amerananisha rushwa na nini?
  3. Madhara gani yanaweza kutokea endapo mtu atatoa au kupokea rushwa?
  4. Kwa nini watu hutoa rushwa?
  5. Kutokana na mazungumzo uliyoyasikiliza, lugha ya mazungumzo ina sifa gani?

Zingatia

Mazungumzo huhusisha pande mbili za mawasiliano, yaani mzungumzaji na msikilizaji. Msikilizaji anapaswa kupata taarifa kwa kusikiliza kwa makini mazungumzo au habari anayosomewa au anayosimuliwa. Habari inaweza kusimuliwa ana kwa ana au kutoka kwenye televisheni, redio, kompyuta, au simu ya mkonomi.

Ili kuelewa vizuri mazungumzo au habari anayosikiliza, msikilizaji anatakiwa:

  1. Kuwa makini - kwa kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili aweze kusikia vizuri na kupata ujumbe uliokusudiwa.
  2. Kubainisha mambo muhimu - andika mambo muhimu tu kutoka kwenye habari anayoisikiliza.
  3. Kumtazama usoni mzungumzaji - ili aweze kupata taarifa za ziada ambazo mzungumzaji anaweza kutoa kwa kutumia ishara za mwili.
  4. Kuwa makini na sarufi ya lugha - na lafudhi ya mzungumzaji.

Lugha ya mazungumzo huwa na sifa zake kadhaa:

  • Kupeana nafasi wakati wa kuzungumza ili mzungumzaji na msikilizaji waweze kusikilizana na kuelewana.
  • Kutumia lugha ya mkato kwa lengo la kurahisisha mawasiliano na kuokoa muda.
  • Matumizi ya ishara na mwongozo wa viungo vya mwili kama vile kukubali, kukataa, kuita na hata kutembea.
  • Urudiaji wa maneno au sentensi kwa lengo la kusisitiza, kufafanua au kutaka kufahamu jambo kwa kina.
  • Matumizi ya wazi ya kiimbo na mkazo ambayo hutumiwa na mzungumzaji kulingana na lengo la ujumbe.
  • Matumizi ya lugha ya vionjo ambayo hufanywa na mzungumzaji na msikilizaji kwa lengo la kuonesha hisia zao.

Zoezi la 4.1

  1. Andika kwa kirefu maneno yaliyokozwa wino katika ngonjera uliyoisikiliza.
  2. Kifungu cha maneno "mti mkavu" ni sehemu ya methali ipi na methali hiyo ina maana gani?
  3. Eleza maana ya nahau "kuzunguka mbuyu" kama ilivyotumika katika ngonjera uliyoisikiliza.
  4. Bainisha maneno yaliyojirudiarudia kutoka kwenye ngonjera uliyoisikiliza.
  5. Unafikiri kwa nini maneno uliyoyabainisha katika swali la 4 yamerudiwarudiwa?

Shughuli ya 4.2

Sikiliza mazungumzo changamani kutoka katika vyanzo mbalimbali, kisha waeleze wanafunzi wenzako mambo yaliyozungumzwa.

Kufupisha mazungumzo changamani

Fupisha hadithi changamani ifuatayo kwa kuzungumza, kisha jibu maswali yanayofuata.

Wavuvi waliiazimika kubadilisha kazi yao kwa takribani miezi miwili. Hii lilitokana na mtumbwi wao kuharibika na kuanza kuingiza maji mengi kupitia mianya iliyokuwa imejitokeza kwenye maungio ya mbao zake. Ingawa kulikuwa na upo mzuri wa kufanyia kazi waliokuwa wakiutumia, uingiaji wa maji ulikuwa mkubwa mno. Uingiaji huo wa maji ulifanya kazi ya kukumba maji hayo isiwezekane. Kwa kweli, tatizo hilo lilitokana na uzembe wao wenyewe. Kama wangechukua hadhari mapema, tatizo hilo lisingekuwa kubwa kiasi hicho. Wahenga walisema usipoziba ufa utajenga ukuta. Kutokana na hali hiyo, ilibidi mtumbwi usimamishwe kufanya kazi ili ukalafatiwe kwanza. Hata hivyo, kazi yenyewe ya ukalafati haikuwa kubwa na isingeweza kuchukua muda mrefu kiasi hicho, lakini kuliibuka mushikeli. Fundi aliyekuwa anafanya kazi hiyo aliishiwa na kalafati ikabidi waagize nyingine kutoka Tanga. Baada ya kalafati kuletwa, fundi alibaini kuwa mtumbwi ulikuwa umcoza na haufai tena kukalafatiwa. Kutokana na mtumbwi kushindikana kutengenezwa, shughuli ya uvuvi ilishia njiani.

Walianza kufanya kazi nyingine ya kununua ng'ombe na kuuza. Walizunguka usiku na mchana vijijini kutafuta ng'ombe kwa wafugaji. Aidha, walianza kuhamia kule walikokuwa wakienda kutafuta ng'ombe kwa matumaini kwamba wangepata ng'ombe wengi zaidi; lakini wapi! Hawakupata ng'ombe wengi kama walivyotarajia na baadhi yao waliandamwa na magonjwa. Wajasiriamali hao walianza kurudi kule walikozoea, ambako siku zote kulikuwa hakuwatupi mikono, kwani biashara ya kuuza mifugo ilikuwa ngumu. Katika uvuvi walikuwa wakiambulia chochote kama wahenga wanenavyo, "Jembe halimtupi mkulima." Waliamua kurudi kwenye uvuvi ambao waliuzoea na kuacha kufanya biashara ambazo hawana uzoefu nazo. Wavuvi hao walifanikiwa kupata samaki si haba.

Maswali

  1. Hadithi uliyoisoma inahusu nini?
  2. Kwa nini zoezi la ukalafati lilishindikana?
  3. Unafikiri mwandishi alimaanisha nini aliposema, "Jembe halimtupi mkulima" na "Usipoziba ufa utajenga ukuta"?
  4. Kwa nini wajasiriamali waliamua kuacha kununua na kuuza ng'ombe na kurudia shughuli ya uvuvi wa samaki?
  5. Ungekuwa wewe ni mvuvi ungewashauri nini watu wengine kuhusiana na shughuli ya uvuvi?

Mfano wa Ufupisho:

Ufupisho wa hadithi: Wavuvi walilazimika kubadilisha kazi yao baada ya mtumbwi wao kuharibika. Walijaribu kukalafati mtumbwi lakini uligundulika kuwa umcoza. Walianza biashara ya ng'ombe lakini walikosa mafanikio. Mwishowe walirudi kwenye uvuvi ambao walijua vizuri na wakafaulu.

Zingatia

Unapaswa kuzingatia kwa makini lugha iliyotumiwa unapotoa ufupisho wa mazungumzo au habari uliyoisikiliza au kuisoma. Katika kufanya hivyo, unapaswa:

  • Kutafuta maneno mengine yanayoweza kutumika badala ya fungu fulani la maneno au badala ya sentensi nzima.
  • Kuangalia mambo muhimu yanayojitokeza katika habari ili usipunguze ujumbe unaotolewa.
  • Kuepuka kuondoa maneno ya msingi ambayo yamo katika masimulizi au habari.

Mifano ya ufupishaji:

  • Fungu la maneno "embe, chungwa, ndizi, chenza, tufaa, na nanasi" yanaweza kufupishwa kwa kusema "matunda."
  • Sentensi "Alitembea polepole kuelekea shuleni akiwa amechukua muda mrefu" inaweza kufupishwa kuwa "Aliwahi kufika shuleni."

Shughuli ya 4.3

Sikiliza kwa makini mazungumzo kuhusu taarifa ya michezo kutoka katika vyanzo mbalimbali vya habari, kisha eleza kwa muhtasari ulichokisikiliza.

Kushiriki katika majadiliano ya miktadha mbalimbali

Wasikilize wanafunzi wenzako wanaposoma dayologia ifuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Nanzia:
(Akitabasamu huku akimtazama rafiki yake.) Heel Helena! Helena habari za likizo?
Helena:
Ni nzuri Nanzia.
Nanzia:
Habari za Masasi?
Helena:
Nzuri pia rafiki yangu.
Nanzia:
Jamani poleni kwa mafuriko, yanatisha!
Helena:
Usiseme Nanzia. Mafuriko yanatisha. Tulifikiri ni kama ...
Nuru:
(Akiidakia.) Enhe! Hebu tusimulie dada.
Helena:
Hapo kwetu ndipo hasa mkondo wa maji ulipopitia. Ilikuwa bahati kwani mzee mmoja aliwahi kupiga kelele tukatoka nje kabla ya balaa lile halafu tukakimbilia kwenye mwinuko.
Nanzia:
Ilikuwa usiku au mchana?
Helena:
Usiku, kama saa tano au sita hivi kwa sababu tulikuwa tumekwishalala.
Nuru:
Yaani nilikimbia?
Helena:
Yule mzee aliwahi kuyaona yale maporomoko ya mawe na miti na maji mengi yakitiririka kutoka milimani …
Nuru:
Jamani Helena, mawe na miti?
Helena:
Eee! Mawe makubwa yaliviringishwa nayo yakavunja miti huku maji yakimong'onyoa ardhi. Chochote kilichokutwa na maji hayo kilisombwa. Gari la misheni ilikumbwa, likasombwa na kuharibiwa kabisa. Basi, maji yale yalipofika kijijini kwetu, Loo!
Nanzia:
(Akishika midomo kwa masikitiko.) Nyumba zenu?
Helena:
Nyumba zetu zilifagiliwa tukiziona hivihivi kwa macho yetu. Vitu vyote vilisombwa tukabaki hivihivi bila hata bakuli, sufuria wala kijiko …
Nuru:
(Akiwa ameshika kichwa.) Helena unasema kweli? Sasa ikawaje?
Nanzia:
Sasa wewe na ndugu zako mnalala wapi?
Helena:
Wee! Tulipata shida. Tulilala nje. Tulikata miti tukatengeneza wigo. Baada ya siku mbili tatu tuliletewa mahema na misaada mingine.
Nanzia:
Jamani Helena! Poleni sana. Tulipopata habari za mafuriko, tulikukumbuka na kukusikitikia.
Helena:
Asante sana rafiki yangu.

Maswali

  1. Mafuriko yanayozungumziwa yalitokea wilaya gani?
  2. Kwa nini Helena alifikiri mafuriko ni kiama?
  3. Dayolojia uliyoisikiliza inahusu nini?
  4. Ni funzo gani ulilolipata kutokana na mazungumzo uliyoyasikiliza?

Mbinu za Kushiriki Katika Majadiliano

1. Usikivu Mkubwa

Zingatia kinachozungumzwa ili uelewe na uweze kuchangia hoja mwafaka.

2. Kuandaa Cha Kusema

Katika mazingira rasmi, andaa hoja zako mapema ili utoe hoja nzito na zinazoeleweka.

3> Kuzingatia Sifa za Lugha ya Mazungumzo

Tumia Kiswahili fasaha na utamkaji sahihi katika majadiliano.

4. Kuheshimu Mwenye Kusema

Toa nafasi ya kuzungumza kwa wengine na usimkasirishe mwenye kusema.

5. Kuwa na Uwazi

Toa maelezo yaliyo wazi na yanayoeleweka kwa wote.

Zingatia

Majadiliano ni njia mojawapo ya kufanya mawasiliano baina ya wazungumzaji. Katika majadiliano, pande zote mbili, yaani mzungumzaji na msikilizaji, huwa na nafasi zote mbili yaani kuwa mzungumzaji na kuwa msikilizaji. Majadiliano huweza kuwa na washiriki wawili au zaidi, ambapo kila mmoja ana nafasi ya kusikiliza na kuzungumza katika kutoa hoja, kufafanua au kuchangia hoja.

Aghalabu, majadiliano huwa na mada maalumu ambazo washiriki husika wanaweza kuamua. Huweza kuwa na mada moja au zaidi. Aidha, majadiliano yanaweza kuwa rasmi au yasiyo rasmi. Hii ina maana kwamba majadiliano yanaweza kuandaliwa rasmi na mada zikabainishwa mapema au yakaibuka tu miongoni mwa wazungumzaji, hasa katika mazingira yasiyo rasmi kama vile katika vijiwe vya vijana, vijiwe vya kahawa au nyumbani.

Ikiwa ni mazingira rasmi, ni vyema kuandaa cha kusema ili utoe hoja nzito na zinazoeleweka kwani utakuwa umeshaijua mada. Hata hivyo, maoni na hoja nyingine huibuka kadiri unavyosikiliza mjadala wa jambo. Jambo la kukumbuka ni kwamba, unapaswa kuzingatia sifa za lugha ya mazungumzo katika majadiliano, utamkaji sahihi na matumizi ya Kiswahili fasaha. Aidha, unapaswa kujua kuwa majadiliano yanahitaji usikivu mkubwa ili uelewe kinachozungumzwa na kuchangia hoja mwafaka. Hivyo, kanuni za usikilizaji mzuri zinapaswa kuzingatiwa.

Shughuli ya 4.4

Fanya majadiliano na wenzako kuhusu ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko. Zingatia sifa za lugha ya mazungumzo na taratibu za majadiliano.

Zoezi la Marudio la 4

1. Oanisha maana ya dhana katika Orodha A na dhana zinazohusika kutoka Orodha B kwa kuchagua herufi ya jibu sahihi.

Orodha A Orodha B
(i) Redio, televisheni, kompyuta, simu ya mkonomi na kinasa sauti A. Kupunga, kukunja uso, kucheka
(ii) Kueleza jambo kwa maneno machache bila kupoteza maana B. Vifaa vinavyoweza kutumika katika mawasiliano ya mazungumzo
(iii) Ishara zitumikazo katika mazungumzo C. Mzungumzaji na msikilizaji
(iv) Mazungumzo huhusisha pande mbili D. Ufupisho
(v) Hutambulisha jamii fulani E. Lafudhi
F. Mkazo
G. Lugha ya mazungumzo

2. Eleza mambo matano (5) yanayoweza kukusaidia kuelewa unaposikiliza mazungumzo.

3. Sikiliza kifungu cha habari kifuatacho kinachosomwa na mwenzako, kisha kifupishe kwa sentensi zisizozidi tano (5).

Wakazi wa Kijiji cha Janda, mkoani Katumbarazi, wameamua kushirikiana kujenga malweni kwa ajili ya shule ya sekondari iliyoko kijijini kwao. Akiongea kwa bashasha katika hafla ya kuzindua malweni hayo, Mkuu wa Mkoa wa Katumbarazi, Brigedia Chekero Rukweche, amewashukuru wanakijiji hao kwa kuona umuhimu wa kujenga malweni. Wanafunzi hao walikuwa wakihangaika kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na kurudi nyumbani. Jumla ya malweni manne yamekamilika, ambapo mawili yatatumiwa na wavulana na mawili yatatumiwa na wasichana. Ujenzi wa malweni hayo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 150.9, ambazo ni michango iliyotolewa na wanakijiji hao sambamba na nguvukazi.

4. Kwa kutumia vifaa vya TEHAMA au kamusi, eleza maana za maneno yafuatayo:

  1. takribani
  2. kukumbuka
  3. hadhari
  4. kalafati
  5. mushikeli
  6. chapusha
  7. wajasiriamali

5. Fanya majadiliano na wenzako darasani kuhusu chanzo cha mnomonyoko wa maadili kwa vijana na kupendekeza nini kifanyike ili kuondoa hali hiyo. Kisha, andika ufupisho wa mjadala huo kwenye daftari lako kwa maneno yasiyozidi 150.

Stadi za Kusikiliza Kwa Ufanisi

Vipengele Muhimu vya Kusikiliza Kwa Makini

1. Kuwa na Kusudi

Jua kwa nini unamsikiliza mzungumzaji - je, ni kwa ajili ya kujifunza, kufurahia, au kuchukua hatua fulani?

2. Kuwa Makini

Toa umakini wako wote kwa mzungumzaji. Epuka vipingamizi vya nje kama vile kelele, simu, au mazungumzo ya wengine.

3. Kuwa na Uvumilivu

Msa mzungumzaji amalize mawazo yake kabla ya kuchangia. Usikaribie hitimisho mapema.

4. Kuwa na Ufunguo

Andika mambo muhimu unayoyasikia ili ukumbuke baadaye.

5. Kuuliza Maswali

Ikiwa huelewi jambo fulani, uliza ili upate ufafanuzi zaidi.

6. Kuakisi

Rudia kwa maneno yako mwenyewe ulichokisikia ili kuhakikisha umeelewa vyema.

Faida za Kusikiliza Kwa Makini

  • Hukuza uelewa wa kina wa masuala mbalimbali
  • Hukuza uwezo wa kujifunza na kukumbuka
  • Huimarisha mahusiano bora na wengine
  • Hupunguza makosa yanayotokana na kutoelewa
  • Hukuza heshima na ujasiri katika mawasiliano
  • Husaidia katika kutatua matatizo kwa ufanisi zaidi
Sura ya Tano: Kusoma kwa Ufasaha na Ufahamu

Sura ya Tano: KUSOMA KWA UFASAHA NA UFAHAMU

Utangulizi

Uelewa wa jambo huweza kutokana na kusoma matini mbalimbali. Katika sura hii utajifunza kusoma kwa ufasaha na ufahamu matini fupi changamani kwa kuzingatia alama za uandishi, kasi stahiki na kiimbo sahihi cha tungo na kueleza athari zake katika usomaji.

Aidha, utajifunza kuandika hoja kuu kutoka katika matini ulizozisoma na kutumia vifaa vya TEHAMA kutafuta maana za maneno. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kupata maarifa na ujuzi wa kufafanua mambo mbalimbali uliyoyasoma. Vilevile, utaweza kuyachambua na kuyapanga mawazo kinantiki. Aidha, utaweza kuandika muhtasari wa kile ulichokisoma.

Fikiri: Namna unavyoweza kupata maarifa ya masuala mbalimbali

Kusoma matini fupi changamani kwa kuzingatia alama za uandishi, kasi stahiki na kiimbo

Soma masimulizi yafuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Kabula:
Habari za kujisomea marafiki zangu!
Nyamizi, Mashaka na Maisha:
Nzuri (Waliitikia kwa pamoja.)
Kabula:
Leo nimesoma kitabu kinachohusu utamaduni wetu. Nimejifunza kwamba kila kabila katika nchi yetu lina utamaduni wake ambao huongoza maisha ya kila siku ya watu wa kabila hilo.
Nyamizi:
Eeeh! Utamaduni huo ni tofauti na utamaduni tuliojifunza katika somo la Kiswahili?
Kabula:
Ndiyo! Kitabu nilichosoma kimezungumzia kuhusu makabila mbalimbali yanayopatikana nchini Tanzania, vyakula vyao vya asili, nyimbo zao pamoja na shughuli nyingine za kitamaduni walizo nazo.
Mashaka:
Kumbe! Leo ndiyo ninasikia kuwa kila kabila lina utamaduni wake. Nilidhani utamaduni wa Watanzania ni mmoja na unatumika katika makabila yote nchini Tanzania. Basi nitaomba uniazime kitabu hicho ili na mimi nikajisomee.
Kabula:
Sawa Mashaka, nitakuazima ukajisomee mwenyewe ili uelewe zaidi kuhusu tamaduni za makabila mbalimbali yaliyopo Tanzania.
Maisha:
Mimi pia ninataka niwaeleze niliyoyasoma katika gazeti. Mimi nimesoma namna ya kupika keki. Gazeti hilo limeeleza jinsi ya kuchanganya viambaaupishi vinavyohitajika katika kupika keki. Nikifika nyumbani nitamwomba mama aninunulie vifaa vyote vya kupikia keki ili nijaribu kupika kama walivyoelekeza katika gazeti. Nikiweza kabisa, nitaanza kupika keki kwa ajili ya kuuza.
Kabula:
Umewaza vyema sana Maisha. Keki ni biashara nzuri sana. Watu wengi hununua keki kwa ajili ya kula wakati wa kusherehekea kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwao, harusi, ubatizo, maulidi na sherehe nyinginezo. Kwa hakika, magazeti yanafundisha mambo mengi sana. Hivyo, sisi sote tuwe na tabia ya kusoma magazeti.
Nyamizi na Mashaka:
Sawa kabisa; tumekuelewa Kabula.
Maisha:
Naona muda wa kurudi darasani umewadia. Turudi darasani tukajiandae kwa ajili ya kipindi cha Kiswahili kabla mwalimu hajaingia. Mashaka na Nyamizi mtamalizia kutusimulia mliyoyasoma wakati tunarudi nyumbani.

Maswali

  1. Masimulizi uliyoyasoma yanahusu nini?
  2. Kutokana na masimulizi uliyoyasoma, Kabula alisoma kitabu kilichohusu nini?
  3. Kuna faida gani ya kusoma matini mbalimbali?
  4. Unafikiri Maisha alitaka anunuliwe viambaaupishi gani vya kupikia keki?
  5. Je, ulishawahi kusoma kitabu, jarida au gazeti lolote? Lilihusu nini? Wasimulie wenzako ulichokisoma.

Mbinu za Kusoma kwa Ufasaha

1. Matamshi Sahihi

Hakikisha unatamka maneno kwa usahihi kulingana na kanuni za lugha ya Kiswahili.

2. Kuzingatia Alama za Uandishi

Zingatia alama kama nukta, alama ya kuuliza, alama ya mshangao, nk.

3. Kasi Stahiki

Soma kwa kasi inayofaa - si haraka sana wala polepole sana.

4. Kiimbo Sahihi

Badilisha kiimbo kulingana na aina ya sentensi - swali, maelezo, amri, nk.

5. Mitiririko wa Aya

Elewa uhusiano kati ya aya na kusoma kwa mtiririko unaofaa.

6. Mkazo wa Maneno

Zingatia silabi zenye mkazo katika maneno ili kupata maana sahihi.

Zingatia

Kusoma kwa ufasaha ni kusoma matini kwa usahihi kwa kuzingatia taratibu za uandishi. Ili msomaji aweze kusoma kwa ufasaha anapaswa kuzingatia matamshi sahihi ya maneno, alama za uandishi, kasi stahiki, mitiririko wa aya, utamkaji sahihi wa silabi zenye mkazo katika maneno pamoja na kiimbo ili kupata maana sahihi.

Kusoma kwa ufahamu ni uwezo wa kusoma na kuelewa jambo fulani lililoandikwa. Mtu anaweza kupata ufahamu kutokana na kusoma kifungu cha habari, makala, matini, kitabu au gazeti. Msomaji anapaswa kuzingatia hatua za usomaji ambazo ni kusoma matini kwa sauti au kimya, kurudia kusoma matini hiyo kwa makini na kubainisha mambo ya msingi yaliyomo katika matini aliyoisoma ili aelewe yaliyomo katika matini. Aidha, anapaswa kuwa makini katika kutafakari jambo alilolisoma ili aweze kutoa taarifa iliyo sahihi au kujibu maswali kwa usahihi.

Msomaji akiwa na ufahamu juu ya jambo fulani anaweza kutoa taarifa yake kwa muhtasari, kwa kuzungumza au kwa kuandika. Katika kusoma kwa ufahamu, msomaji anapaswa kufahamu matini anayoisoma inahusu nini, yaani mawazo makuu yanayoelezwa. Aidha, msomaji anapaswa kubaini maneno mapya yaliyotumika katika matini aliyoisoma na namna yaliyotumika. Kufanya hivyo, kutamsaidia kutambua lengo la mwandishi.

Hivyo, ili kusoma kwa ufasaha na ufahamu, msomaji anatakiwa kuwa makini kwa kuelekeza fikra zake katika kile anachokisoma ili aweze kupata uelewa wa kina katika kila anachokisoma. Kusoma kwa ufasaha na ufahamu ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku kwa kuwa hutuwezesha kukuza uelewa wa mambo mbalimbali na stadi za kuzungumza na kuandika. Vilevile, hukuza uwezo wa kujenga hoja juu ya mambo mbalimbali na kujieleza kwa ufasaha na kwa ufupi. Aidha, hukuza uwezo wa kuchambua mambo anuai na kuchochea ari ya kujisomea.

Zoezi la 5.1

  1. Eleza mambo ya kuzingatia wakati wa kusoma matini kwa sauti.
  2. Andika kifungu cha habari kisichozidi maneno hamsini (50) kuhusu tukio lolote kwenye gazeti au matini yoyote, kisha ukisome kifungu hicho.

Umuhimu wa alama za uandishi na kiimbo katika usomaji

Soma hadithi ifuatayo kwa kuzingatia alama za uandishi, kasi stahiki na kiimbo sahihi, kisha jibu maswali yanayofuata.

Bota ni mtoto wa kiume katika familia ya Mzee Bure aliyezaliwa na kulelewa katika mazingira ya kijijini. Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, hakubahatika kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa kuwa hakufanya vizuri katika mitihani yake. Suse, mama yake Bota, alimshauri mume wake wampeleke kijana wao katika shule binafsi ili aweze kupata elimu ya sekondari. Bure alionesha kusita kwa kuwa hakuwa na uwezo mzuri wa kifedha. Hata hivyo, kutokana na ushawishi wa mkewe, alikubali ushauri huo na akauza ng'ombe mmoja aliyekuwa naye kisha akampeleka mtoto wake shuleni.

Kutokana na hali ya uchumi kuwa ngumu, wakati mwingine Bota alichelewa kwenda shuleni kwa sababu ya kukosa ada. Mama yake aliumizwa sana na hali hiyo; hivyo, akaamua kuanzisha biashara ya kuchuuza samaki. Aliuza samaki hao kwa kubadilishana na mazao kisha akauza mazao hayo na kujipatia fedha. Kila faida aliyoipata alitelekeza katika kumsomesha Bota. Baba yake pia alijitahidi kufanya kazi zake kwa bidii ili kwa pamoja, wapate fedha za kumsomeshea mtoto wao. Maisha yalizidi kuwa magumu kwani kuna wakati walikula mboga bila chumvi na kuoga bila sabuni ili tu Bota apate ada na mahitaji ya shule.

Baada ya kuhitimu kidato cha nne, Bota alichaguliwa kujiunga na chuo cha uvuvi ambako alihitimu mafunzo yake. Alipomaliza, hakusubiri kuajiriwa na serikali bali aliamua kujiunga na kikundi cha vijana wajasiriamali. Alichukua mkopo kwenye kikundi chake akanunua zana za uvuvi na kuamua kujiajiri kwenye sekta ya uvuvi.

Mungu si Athumani, biashara ya uvuvi ilimletea tija kwani Bota alipata mtaji mkubwa wa kiasi cha kuweza kusafirisha samaki ndani na nje ya nchi. Maisha yake na ya familia yake yalibadilika na kuwa mazuri. Aliweza kupata fedha za kuwajengea wazazi wake nyumba nzuri na kununua gari. Wazazi wake walikumbuka maisha ya awali na kusema, "Ama kweli mchumia juani hulia kivulini."

Maswali

  1. Hadithi uliyoisoma inahusu nini?
  2. Kama ungekuwa mzazi wa Bota, ungefanya nini baada ya Bota kutokuchaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari?
  3. Umejifunza nini kutokana na hadithi uliyoisoma?
  4. Ukipewa nafasi ya kushauri, utawashauri nini wahitimu wanaosubiri kuajiriwa?
  5. Kwa kutumia kamusi au vyanzo vya mkondoni vinavyoaminika, eleza maana za maneno yaliyokozwa wino kama yalivyotumiwa katika hadithi uliyoisoma.

Alama za Uandishi na Matumizi Yake

1. Nukta (.)

Hutumiwa kuonesha mwisho wa sentensi ya maelezo au amri.

Mfano: Bota alihitimu mafunzo yake.

2. Alama ya Kuuliza (?)

Hutumiwa mwishoni mwa sentensi ya swali.

Mfano: Unakwenda wapi?

3. Alama ya Mshangao (!)

Hutumiwa kuonesha mshangao, furaha, hasira au hisia kali.

Mfano: Lo! Gari limeharibika!

4. Mkato (,)

Hutumiwa kutenganisha vitu kwenye orodha, sehemu za sentensi, nk.

Mfano: Alinunua embe, machungwa, na ndizi.

5. Nukta Pacha (:)

Hutumiwa kutaja orodha au kutoa maelezo.

Mfano: Anahitaji vitu vitatu: kalamu, daftari na kitabu.

6. Nukta Mkato (;)

Hutumiwa kuunganisha sentensi zinazohusiana.

Mfano: Alikwenda mjini; hakuwa na pesa.

Zoezi la 5.2

Tumia alama za uandishi kuonesha kiimbo stahiki kwa kila sentensi.

  1. Marafiki wawili walikuwa wakitembea bustanini
  2. Ghafla Mvua ilianza kunyesha
  3. Mvua ilipokuwa inaendelea kunyesha walimwona mbwa mdogo akiwa amelowa na hajitambui
  4. Mbwa huyo alikuwa akitetemeka sana
  5. Marafiki hao walimchukua mbwa huyo haraka na kwenda naye nyumbani kwao
  6. Baada ya kufika nyumbani, walimpa chakula na maji na kukaa naye karibu na moto ili apate joto
  7. Mbwa huyo hakurudi tena porini
  8. Waliishi na mbwa huyo hadi wakamzoea

Athari za alama za uandishi na kiimbo katika usomaji

Soma kifungu cha habari kifuatacho, kisha jibu maswali yanayofuata.

Kijiji cha Umoja ni maarufu kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika kijiji hicho kulikuwa na bwawa maarufu lillioitwa Majani Mapana wakazi wa eneo hilo walilitumia bwawa hilo katika shughuli zao za umwagiliaji kijiji hicho kilikumbwa na ukame baada ya mvua kukosekana kwa muda mrefu Wakulima katika kijiji hicho waliathiriwa sana na hali hiyo Walilalamika juu ya upungufu mkubwa wa maji katika bwawa hilo walijiuliza tufanye nini ili kuepuka adha hii maisha yetu yatakuwaje walijiuliza maswali hayo kwa kuwa hali hiyo ilisababisha kushuka kwa uchumi wao

Maswali

  1. Umepata changamoto gani katika kusoma kifungu cha habari ulichopewa?
  2. Andika kifungu hicho cha habari kwa kuzingatia alama za uandishi.
  3. Alama zipi za viimbo zimekosekana katika kifungu cha habari ulichokisoma?
  4. Soma kwa sauti kifungu cha habari ulichokirekebisha.

Kifungu Kilichorekebishwa:

Kijiji cha Umoja ni maarufu kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Katika kijiji hicho kulikuwa na bwawa maarufu lillioitwa Majani Mapana. Wakazi wa eneo hilo walilitumia bwawa hilo katika shughuli zao za umwagiliaji.

Kijiji hicho kilikumbwa na ukame baada ya mvua kukosekana kwa muda mrefu. Wakulima katika kijiji hicho waliathiriwa sana na hali hiyo. Walilalamika juu ya upungufu mkubwa wa maji katika bwawa hilo. Walijiuliza, "Tufanye nini ili kuepuka adha hii? Maisha yetu yatakuwaje?" Walijiuliza maswali hayo kwa kuwa hali hiyo ilisababisha kushuka kwa uchumi wao.

Zingatia

Kusoma kwa ufahamu na ufasaha huzingatia matumizi sahihi ya alama za uandishi kama vile: (,) (!), (.), (:), (?), (…), (" "), (') na (;), pamoja na kiimbo. Kuna umuhimu mkubwa wa kuzingatia alama za uandishi katika usomaji wa habari, hadithi au matini yoyote.

Ni muhimu kuzingatia alama za uandishi kwani husaidia kutenganisha au kuunganisha maneno na kuonesha mwisho wa sentensi. Pia, ni muhimu kuzingatia matumizi ya herufi kubwa katika utumiaji wa alama za uandishi. Aidha, kiimbo husaidia kuonesha lengo la mwandishi katika matini husika. Mwandishi anaweza kutumia kiimbo kwa lengo la kuuliza swali, kutoa maelezo, kutoa amri au kuonesha hisia za mwandishi.

Alama za uandishi na kiimbo ni muhimu kwa kuwa huwafanya wasikilizaji au wasomaji wa habari waelewe kwa ufasaha kile kinachosomwa. Kutokuzingatia usahihi wa matumizi ya alama hizo hufanya ujumbe kupotea au habari kutoa maana tofauti. Hivyo, kutokuzingatia kiimbo huleta athari kwenye ujumbe wakati wa usomaji wa matini.

Shughuli ya 5.1

  1. Soma kifungu cha habari ulichopewa.
  2. Andika upya kifungu cha habari utakachokisoma kwa kufuata taratibu za uandishi zifuatazo:
    1. kichwa cha habari
    2. aya
    3. alama za uandishi
    4. matumizi sahihi ya herufi kubwa

Kuandika hoja kuu kutoka katika matini fupi changamani

Soma habari ifuatayo, kisha bainisha mawazo makuu ya habari hiyo.

Wakapita nyika, pululu na tambarare kwenye eneo la Safu ya Milima ya Usambara. Walipokaribia eneo la Mto Wami, walikabiliana na lori refu la kubebea shehena nzitonzito. Lori hilo liliokuwa linatokea Dar es Salaam kuelekea Arusha liikuwa limewasha taa mchana. Liikuwa likija kwa kasi huku likiyumbayumba barabarani. Dereva wa daladala iliyokuwa inaelekea Chalinze aling'amua ghafla kwamba mambo ni tenge tahanani. Alijaribu kukikwepa kichwa cha lori kilichokuwa kimemkodolea macho kama simba wa hifadhi ya wanyama ya Serengeti bila mafanikio. Alikuwa amechelewa mno.

Lori ile lilikwangua daladala na kuirarua. Ulisikika milo, kwa-ka-ra-kwa-ka-ra, pfyuuuuuuu! Likapita juu ya ile daladala na kwenda kuyafukunyua magari mengine sita yaliyofuatana na daladala hiyo. Vyuma vilikutana na vyuma, mabati yakaumana na mabati na viungo vya watu kumenyeka na kukatika. Kufumba na kufumbua, wingu la vumbi lilikuwa limetanda barabarani.

Baadhi ya wanahabari waliokuja kupiga picha walijikuta wamelazwa hospitalini kwa mshtuko kutokana na mandhari yale ya kutisha. Walikuwa hawajawahi kuona mkasa mbaya kama huo barabarani. Watu arobaini walifariki papo hapo na wengine kumi na watatu walijeruhiwa. Baadhi ya majeruhi waliumizwa vibaya sana.

Mwenyekiti wa Chama cha Nyumbani alinusurika na alionekana pasi kupata jeraha lolote. Alionekana akikimbia huku na kule kuwaokoa majeruhi na kuopoa maiti. Walionwona akijumuika na wenyeji wa eneo la tukio katika uokoaji wanasema hakuonesha kujeruhiwa; isipokuwa uchovu tu. Alisimama ghafla akajishika nyongani na kusema, "Jamani ni muhimu kuzingatia suala la kasi katika uendeshaji wa vyombo vya usafiri na sheria nyingine za barabarani."

Mbinu za Kuandika Muhtasari

1. Kusoma Kwa Makini

Soma matini yote kwa makini na kuelewa wazo kuu.

2> Kutambua Wazo Kuu

Bainisha wazo kuu la matini na mawazo muhimu yanayosaidia.

3. Kuondoa Maelezo Yasiyo Muhimu

Acha maelezo yasiyo ya msingi na yale yanayorudiwarudia.

4. Kutumia Maneno Yako Mwenyewe

Andika kwa kutumia lugha yako mwenyewe bila kupoteza maana ya asili.

5. Kuweka Mtiririko

Hakikisha muhtasari wako una mtiririko mzuri na unaoeleweka.

6. Kuangalia Urefu

Hakikisha muhtasari wako una urefu unaofaa na haukosi mambo muhimu.

Zingatia

Kuandika hoja kuu ni kutoa muhtasari wa kile kilichokusudiwa kuelezwa katika matini uliyoisoma. Ili kuweza kuandika hoja kuu kutokana na matini yoyote ile, msomaji hana budi kusoma matini nzima na kutelewa barabara. Lengo la kutoa muhtasari ni kukuza uwezo wa kupambanua mawazo muhimu yanayotokana na kusoma au kusikiliza na kuyapanga kinantiki.

Katika kuandika hoja kuu, mwandishi anapaswa kuandika maelezo kwa maneno yake mwenyewe pasipo kupoteza maana ya msingi. Uandishi wa hoja kuu husaidia katika kutayarisha na kuwasilisha ripoti na taarifa mbalimbali kwa kuandika mambo muhimu kwa muhtasari.

Shughuli ya 5.2

Soma matini yoyote kutoka katika vyanzo mbalimbali, kisha andika muhtasari wa matini uliyoisoma kwa maneno yasiyozidi hamsini (50).

Kutumia vifaa vya TEHAMA kutafuta maana za maneno

Soma shairi lifuatalo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Badilisha mtazamo, yache ya kukariri,

Maisha yabadilika, wakati unakuta,

Kazi yataka ujuzi, vyeti using'ang'anie,

Hapa kazi ndiyo mbiu, sije jisahaulisha.

Agizo uzingatie, acha randaranda ovyo,

Tumia ujuzi wako, zao la elimu yako,

Kazi fanya kwa bidii, upate mradi wako,

Siku zote zingatia, kujua ni diko kuishi.

Stangalie ya ndugu, wala jirani mzee,

Yeye ajira lipata, kwa hizo zama za nyuma,

Zama zimepinduliva, hilo weka akilini,

Tumia ujuzi wako, upate wako mradi.

Jizatiti tehamani, jopo kwa kasi amua,

Ngamizi mpakatoni, simu janja aminia,

Kinyonyi na redioni, vifaa vyote sawia

Tumia ujuzi wako, upate chako kipato.

Lako pato ukishika, madhila hukuambaa,

Kuku wa John kaibwa, wewe kando utakuwa,

Hayakusumbui nafsi, moyo wako utabwaga,

Usikose zingatia, ujuzi kipaumbele.

Maswali

  1. Shairi hili linahusu nini?
  2. Shairi ulilolisoma lingefaa kuwa na kichwa gani?
  3. Ni ujumbe gani umcupata kutoka katika shairi hili?
  4. Vifaa gani vya TEHAMA vinaweza kutumika kutafuta maana za maneno yaliyokozwa wino katika shairi ulilolisoma?
  5. Kwa kutumia vifaa vya TEHAMA eleza maana za maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika shairi ulilolisoma.
    1. kukariri
    2. randaranda
    3. hukuambaa
    4. utabwaga
    5. kipaumbele

Vifaa vya TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano)

TEHAMA inajumuisha vifaa mbalimbali vinavyoweza kutumika kutafuta maana za maneno na kukuza ujuzi wa lugha:

  • Kamusi za Mtandaoni - Zinapatikana kwenye tovuti mbalimbali
  • Programu za Simu - Programu za kamusi zinazoweza kupakuliwa kwenye simu za mkononi
  • Vidokezo vya Sauti - Vifaa vinavyotoa matamshi sahihi ya maneno
  • Maktaba za Dijitali - Vitabu vya kielektroniki vinavyoweza kusomwa kwenye vifaa vya TEHAMA
  • Programu za Kutafsiri - Zinasaidia kuelewa maana za maneno katika lugha mbalimbali
  • Vyanzo vya Maarifa - Kama Wikipedia na tovuti nyingine za kielimu

Kutumia vifaa hivi kwa ufanisi kunaweza kukusaidia:

  • Kupata maana za maneno mapya haraka
  • Kusikiliza matamshi sahihi ya maneno
  • Kupata mifano ya matumizi ya maneno katika sentensi
  • Kujifunza visawe na kinyume cha maneno
  • Kupanua ujuzi wako wa msamiati

Zoezi la Marudio la 5

1. Chagua jibu sahihi katika maswali yafuatayo:

  1. Dhana ya kusoma kwa ufahamu hufasiliwaje?
    1. Kusoma, kufikiri, na kuelewa jambo au vitu
    2. Kuona, kusikiliza, na kutafakari
    3. Kuwa makini katika kutafakari jambo
    4. Kusoma, kusikiliza, na kuona
    5. Kufikiri, kusoma, na kuona
  2. Alama za uandishi, matamshi sahihi ya maneno na kasi stahiki katika usomaji husaidia nini kwa msomaji?
    1. Kujenga hoja
    2. Kuchochea ari ya kusoma
    3. Kuelewa kile kinachozungumziwa
    4. Kupenda kusoma
    5. Kujiuliza maswali
  3. Adela anatikisa chupa ya dawa ya kikohozi kabla ya kunywa. Unafikiri kwa nini Adela anafanya hivyo?
    1. Alisoma ila hakuelewa maelekezo ya dawa.
    2. Alisoma na alielewa maelekezo ya dawa.
    3. Hakusoma ila alielewa maelekezo ya dawa.
    4. Hakusoma wala kuelewa maelekezo ya dawa.
    5. Alisoma maelekezo ya dawa.
  4. Mambo yapi kati ya yafuatayo huzingatiwa katika kusoma kwa ufahamu na ufasaha?
    1. Kuzingatia matamshi sahihi, alama za uandishi na kubainisha mambo ya msingi.
    2. Kuchochea ari ya kujisomea, kubaini maneno mapya na kuchambua mambo ya msingi.
    3. Kujenga hoja, kujieleza kwa ufasaha na kuchambua mambo anuai.
    4. Kukuza uelewa wa mambo mbalimbali, kubaini maneno mapya na kuchochea ari ya kujisomea.
    5. Kubaini mawazo makuu, kuelewa maneno anayoyasikia na viimbo na kujieleza kwa ufasaha.
  5. Ni kwa namna gani unaveza kuelewa lengo la mzungumzaji katika mazungumzo?
    1. Kwa kuzingatia matamshi sahihi ya maneno
    2. Kwa kutumia alama sahihi za uandishi
    3. Kwa kusikiliza kiimbo cha mzungumzaji
    4. Kwa kutumia maneno maalumu
    5. Kwa kuangalia msamiati

2. Oanisha maelezo yaliyopo katika Orodha A na dhana zilizopo katika Orodha B kwa kuchagua herufi ya jibu sahihi.

Orodha A Orodha B
(i) Kuzingatia habari na kubainisha mawazo makuu na kuyaelewa. A. kusoma kwa sauti
(ii) Nukta, mkato, ritifaa, mshangao, kiulizo, nukta pacha B. kusoma kimyakimya
(iii) Msomaji hufumba kinywa na kupitisha macho kwenye maandishi. C. ufupisho
(iv) Kuimarisha ujuzi wa kutamka kwa kufuata kanuni, na lafudhi ya Kiswahili. D. alama za uandishi
(v) Kuandika kwa muhtasari kwa kuzingatia mawazo makuu katika habari. E. mambo makuu ya kuzingatia katika ufahamu
F. ufahamu
G. kuchambua maandishi

3. Mtu anaweza kupata ufahamu kuhusu masuala mbalimbali kwa njia gani?

4. Bainisha vyanzo mbalimbali vya taarifa na maarifa kuhusu masuala ya kijamii, kiuchumi, kiteknologia na kidiplomasia.

5. Kwa nini kusoma kwa ufahamu ni muhimu katika maisha yetu ya kila siku?

Sura ya Sita: Kuwasiliana kwa Njia ya Mazungumzo

Sura ya Sita: KUWASILIANA KWA NJIA YA MAZUNGUMZO

Utangulizi

Taarifa mbalimbali huweza kutolewa kwa njia ya mazungumzo. Katika sura hii, utajifunza kuwasiliana kwa njia ya mazungumzo kwa kutumia Kiswahili fasaha.

Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kukuza uwezo wa kujieleza kwa ufasaha kwa njia ya mazungumzo katika miktadha mbalimbali. Vilevile, utaweza kujenga mahusiano mazuri miongoni mwa wanajamii.

Fikiri: Unavyoweza kuwasiliana kwa ufasaha kwa njia ya mazungumzo

Kuzungumza kwa ufasaha katika miktadha mbalimbali

Soma na mwenzako dayologia ifuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Daktari:
Habari ya leo? (Anamsalimu kwa uchangamfu.)
Mashaka:
Nzuri! (Anaitikia salamu kwa unyonge.)
Daktari:
Karibu nikuhudumie! Unaonekana munyonge na mwenye mawazo sana. Kulikoni?
Mashaka:
Ninaumwa sana daktari. Kifua kinaniuma na ninakosa hamu ya kula; na kila ikifika jioni, ninapatwa na homa kali inayoambatana na jasho jingi.
Daktari:
Pole sana! Nitakuandikia vipimo vya kwenda maabara na utafanya eksirei. Majibu ya vipimo yakitoka utarudi chumba namba nane.
Mashaka:
Sawa daktari. (Anaelekea maabara kupima vipimo alivyoagizwa na daktari.)
Daktari:
(Baada ya majibu kutoka, Mashaka anatingia katika chumba cha daktari) Karibu tena Mashaka! Majibu yametoka na kipimo cha makohozi kimoonesha kuwa una ugonjwa wa kifua kikuu.
Mashaka:
Anashusha pumzi kidogo! Daktari nitapona kweli? Kwa sababu nilisikia redioni kuwa kifua kikuu kinaua na kwamba tujikinge dhidi ya ugonjwa huo.
Daktari:
Usiwe na hofu Mashaka. Kifua kikuu kinatibika. Ukizingatia matumizi sahihi ya dawa unapona kabisa.
Mashaka:
Unasema kweli daktari?
Daktari:
Ndiyo. Unachotakiwa ni kuacha vitu kama uvutaji wa sigara na matumizi ya pombe katika kipindi hiki cha matibabu, kwani kuendelea kutumia vitu hivyo, kutakufanya uzidi kuathiri mapafu na kudhoofika.
Mashaka:
Sawa daktari nitazingatia. Je, vipi kuhusu familia yangu, nitakuwa nimewaambukiza?
Daktari:
Kifua kikuu kinaambukiza kwa njia ya hewa. Mtu mwenye kifua kikuu akiwa na kikohozi sugu anaweza kuwaambukiza wengine ila wewe umewahi kupata matibabu. Zaidi ya hayo, mtu akishaanza kutumia dawa za kifua kikuu si rahisi kuwaambukiza wengine kwani bakteria wanakuwa wamefubazwa. Hata hivyo, ninashauri na wao wapime.
Mashaka:
Je, ugonjwa huu husababishwa na nini na tunawezaje kujikinga?
Daktari:
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria. Tunaweza kujikinga kwa kuepuka matumizi ya sigara, kuepuka msongamano, mgonjwa kuvaa barakoa, mgonjwa kuanza kutumia dawa na kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa.
Mashaka:
Dalili gani nyingine zinaonesha kuwa mtu anaumwa kifua kikuu?
Daktari:
Ahaaa! Dalili nyingine ni kutoa makohozi yenye damu, kukosa hamu ya kula, mwili kuchoka, kutokwa na jasho kwa wingi wakati wa usiku, kuwa na homa na wakati mwingine mtu kupungua uzito.
Mashaka:
Asante sana daktari, umenielewesha vyema. Nimejifunza mambo mengi kuhusu ugonjwa huu. Nitakwenda kutumia dawa zangu vizuri na kuzingatia maelekezo uliyonipa.
Daktari:
Nami nimefurahi. Utapaswa kufika hospitalini kila mwezi kwa ajili ya kuchukua dawa za kumeza. Nakutakia afya njema na ugua pole.
Mashaka:
Asante sana daktari, nami nakutakia kazi njema.

Maswali

  1. Mazungumzo uliyoyasoma ni ya muktadha gani?
  2. Kutokana na dayolojia uliyoisoma, daktari alimshauri nini Mashaka?
  3. Nini kifanyike ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu?
  4. Unafikiri ni kwa nini Mashaka alipata hofu alipoambiwa na daktari kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu?
  5. Ni funzo gani ulilolipata kutokana na mazungumzo ya daktari na Mashaka? Eleza kwa ufupi kwa njia ya mazungumzo.

Mifano ya Mazungumzo katika Miktadha Tofauti

1. Mazungumzo ya Shuleni

Mwanafunzi:
Shikamoo mwalimu. Samahani kwa kuchelewa kipindi. Nimechelewa kwa sababu mto umejaa maji kutokana na mvua iliyonyesha jana usiku.
Mwalimu:
Oh! Pole sana kwa changamoto hiyo, ingia darasani.
Mwanafunzi:
Asante mwalimu.

2. Mazungumzo ya Marafiki

Rafiki 1:
Aisee! Leo nina furaha sana rafiki yangu.
Rafiki 2:
Kwa nini?
Rafiki 1:
Ule mpango wangu wa kwenda kuchukua mzigo wa biashara umekamilika.
Rafiki 2:
Aisee! Hongera sana.

3. Mazungumzo ya Wavuvi

Mvuvi 1:
Siku hizi samaki wameadimika sana, kwa nini?
Mvuvi 2:
Nimeongea na wavuvi wenzetu tumebaini kwamba kuna shughuli nyingi za uvuvi haramu zinaendelea. Hali hii inasababisha samaki kuadimika kutokana na njia haramu wanazozitumia kuvua.
Mvuvi 1:
Kuna sababu nyingine inayosababisha hali hiyo?
Mvuvi 2:
Ndiyo. Mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri pia upatikanaji wa samaki.

Zingatia

Mazungumzo ni njia mojawapo ya mawasiliano inayomwezesha mtu kujieleza kwa njia ya mdomo. Huweza pia kuambatana na ishara za viungo vya mwili. Chanzo cha mazungumzo ni mzungumzaji na kikomo chake ni msikilizaji.

Ili mazungumzo yafanyike kwa ufasaha, mzungumzaji anapaswa kuzingatia muktadha wa mazungumzo. Mazungumzo yoyote hutegemea muktadha kwani ndio huongoza katika kuchagua msamiati wa kutumia. Muktadha wa mazungumzo unaweza kuwa rasmi au usiwe rasmi; hivyo, msamiati utakootumika utategemea aina ya muktadha unaohusika.

Vilevile, muktadha huhusisha mada inayozungumziwa ambayo pia huamua msamiati wa kutumia katika mazungumzo husika. Aidha, ili mazungumzo yawe fasaha, ni lazima kuzingatia uhusiano baina ya wazungumzaji. Hii husaidia katika kuteua msamiati unaoendana na wazungumzaji ili kufanya mazungumzo yaeleweke.

Kadhalika, mazungumzo fasaha huzingatia hali za wazungumzaji; kwa mfano, kama mzungumzaji ni mgonjwa au amekasirika, lugha inayotumika kuwasiliana naye itaendana na hali hiyo. Lugha inayotumika inapaswa kuendana na hali za wahusika wakati wa mazungumzo ili kuleta maelewano.

Pamoja na hayo, mazungumzo fasaha hutegemea pia shughuli inayohusika. Hii ina maana kwamba, msamiati unaohusika katika mazungumzo huendana na shughuli inayohusika baina ya wazungumzaji; kwa mfano, ikiwa ni kilimo, uvuvi au ufugaji na msamiati wake utaendana na shughuli husika.

Shughuli ya 6.1

Tembelea eneo mahususi kama vile sokoni, kituo cha mabasi, hotelini na hospitalini. Sikiliza mazungumzo ya mahali ulipotembelea na kuchunguza vitu mbalimbali vilivyopo, kisha andaa mazungumzo kutokana na mahali hapo na kuwasilisha darasani.

Kutumia lugha kwa ufasaha katika mazungumzo

Sikiliza ngonjera inayotambwa na wenzako darasani, kisha jibu maswali yanayofuata.

Anita:

Kaka kusanya sahani, walizota wazazi,

Kisha udeki jikoni, halafu menya viazi,

Pia utachanja kuni, ukaazime na mbuzi,

Mimi nakwenda bombani, nitapita na nazi.

Abaya:

Dada nakusihi koma, kazi hizo kazi zako,

Tena kuwa na heshima, viache vyako vituko,

Sifanyi kazi za mama, kwetu wanaume mwiko,

Nakataa ninasema, hata iwe kwa viboko.

Anita:

Hakuna kazi ya kike, wala kazi ya kiume,

Maji kichwani jitwike, nami kuwinda nivume,

Tena jikoni upike, acha kasumba udume,

Na chungu ukainjike, hakuna cha mwanamume.

Abaya:

Mwanamume katafuta, akina dada kupika,

Kuwinda bila kusita, kidume kupapatika,

Sisi kupigana vita, kilimoni kutumika,

Kazi yenu ni kusuta, umbea mmefurika.

Anita:

Ninakupa pole sana, kwayo imani potofu,

Nakueleza bayana, akili kama ya pofu,

Hebu acha kutukana, kuwa kaka mnyoofu,

Acha kabisa kutuna, kujizolea wasifu.

Abaya:

Sijizolei wasifu, nakueleza ukweli,

Ninyi kwetu wahafifu, tepetepe yenu mili,

Hali zenu tahafifu, acha kataa kubali,

Pole kwa kuwakashifu, ila nakupa ukweli.

Anita:

Sisi sote wakulima, mazao tunazalisha

Kila kazi tunavuma, kwa hili acha kubisha,

Viliyyo tunajituma, pengine hadi kukesha,

Masomo tunayasoma, ngazi zote tunatisha.

Ulimwengu katufunda, wayaona maajabu,

Kwa sayansi si makinda, tunapata na majibu,

Imelia parapanda, hatuwezi jitanibu,

Mapambano kwa viwanda, maendeleo jawabu.

Abaya:

Usemacho dada kweli, haupo mfumo dume,

Tupo sawa zetu hali, sote kazi tujiume,

Twajidunisha kimali, eti kisa wanaume,

Kabisa nimekubali, wenzangu tusitutume.

Leo umenifundisha, sasa nitawajibika,

Dhana udume komesha, kazi zote kufanyika,

Si vyombo tu kuviosha, na kupika nitapika,

Jikoni nitasafisha, moyoni sitokwazika.

Chanzo: Uduni wangu: Ngonjera za Watoto (Mbijima, 2020: 10 -11)

Maswali

  1. Ngonjera uliyoisikiliza inahusu nini?
  2. Watambaji wapo katika muktadha gani wa mazungumzo?
  3. Shughuli zipi zimebainishwa katika ngonjera uliyoisikiliza?
  4. Je, una maoni gani kuhusu mada ya ngonjera uliyoisikiliza?

Vipengele vya Lugha ya Mazungumzo Fasaha

1. Usahihi wa Matamshi

Tumia matamshi sahihi ya maneno ili kuepuka kutofautiana kwa maana.

2. Ufasaha wa Lugha

Tumia lugha ya Kiswahili sanifu bila kuchanganya na lugha nyingine isipokuwa kwa sababu maalumu.

3. Ustahiki wa Msamiati

Chagua msamiati unaofaa kulingana na muktadha na hadhira.

4. Kiimbo Sahihi

Zingatia kiimbo kinachofaa kulingana na lengo la mazungumzo.

5> Kasi Stahiki

Zungumza kwa kasi inayofaa - si haraka sana wala polepole sana.

6. Uwazi wa Maelezo

Toa maelezo yaliyo wazi na yanayoeleweka kwa msikilizaji.

Shughuli ya 6.2

Chagua mada moja kati ya zifuatazo, kisha andaa mdahalo kwa kushirikiana na wenzako.

  1. Shule za kutwa ni bora kuliko za bweni
  2. Ualimu ni bora kuliko udaktari
  3. Uchumi wa buluu ni bora kuliko kilimo cha karafi

Mazoezi ya Vitendo

Zoezi la Usaili

Fikiria unataka kugombea nafasi ya kiranja mkuu katika shule unayosoma. Umeitwa kwenye kikao cha usaili na kamati ya shule ya uteuzi. Eleza jinsi utakavyoyajibu maswali yafuatayo:

1. Kwa nini unataka kugombea nafasi hiyo?

2. Ni sifa gani za ziada ulizonazo zinazoweza kukufanya uchaguliwe?

3. Vitu gani utakavyovifanya katika kuleta maendeleo ya shule, hususani katika taaluma?

4. Ikiwa umepata nafasi hiyo na ikatokea mwanafunzi mwenzako amepata changamoto yoyote ya kitaaluma, utaitatuaje?

5. Ni kwa namna gani utahakikisha malengo ya wanafunzi yanafikiwa?

Mada za Majadiliano na Mjadala

Mada 1: Teknolojia na Vijana

Hoja Kuu: Je, matumizi ya teknolojia kwa vijana yanawasaidia au kuwadhuru katika maendeleo yao?

Mada 2: Mazingira na Maendeleo

Hoja Kuu: Je, ni vyema kukata miti ili kujengea viwanda au kutunza misitu kwa ajili ya mazingira?

Mada 3: Elimu ya Msingi

Hoja Kuu: Je, elimu ya msingi inapaswa kuwa ya bure na ya lazima kwa watoto wote?

Mada 4: Kilimo cha Kisasa

Hoja Kuu: Je, ni bora kutumia mbinu za kilimo cha kisasa au kudumisha kilimo cha jadi?

Shughuli ya 6.3

Shirikiana na mwenzako kutunga igizodhima la malumbano ya hoja juu ya "Uchomaji wa Mkaa" na kufanya malumbano hayo.

Zoezi la Marudio la 6

1. (a) Soma shairi lifuatalo, kisha eleza mawazo makuu ya shairi hilo.

Chanjagaa chanjagaa, hiyo enzi ya zamani,

Kajenga nyumba kakaa, hadi leo duniani,

Ipo tena imejaa, kote mwanbao wa pwani,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

Kuna viumbe kadhaa, wapo wanaishi ndani,

Wanaishi kijamaa, kwa makabila si dini,

Wamegawana mitaa, wapo wa juu na chini,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

Kolekole na dagoa, kibua na saradini,

Nyangumi, pweza na taa, mkunga mwenda wa chini,

Wadogo wadogo chaa, na wenye ngozi laini,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

Kusafirisha bidhaa, za bara na visiwani,

Mizigo pia vifaa, vile vya maofisini,

Nahodha nanga hutia, ngalawa ama botini,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

Utalii unafaa, kwenda randa ufukweni,

Wageni kuwavutta, na utalii wa ndani

Maji kupwa na kujaa, ni shani yake manani,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

Kilimo ndiyo hewaa, maarufu sana mwani,

Kinazikidhi kadhaa, kuvua umasikini,

Mawe yake ni sanaa, hupambia majumbani,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

Maji yake yanang'aa, hutupa yote 'fukweni

Uchafu na mabalaa, yanasafisha jueni,

Bahari haina waa, mchanga wake laini,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

Baharini ninakaa, katikati si pembeni,

Si kama nina hadaa, kwa haya sina ugeni,

Nawe kipata wasaa, fanya uje visiwani,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

Nazimaliza karaa, tamati ni kitukoni,

Imeshatimia saa, kalamu naweka chini,

Bado tunajiandaa, gesi na mafuta kwani,

Unuhimu sikieni, bahari nahadithia.

(b) Tunga sentensi kwa kutumia maneno yaliyokozwa wino yaliyotumika katika shairi ulilolisoma.

2. Kwa kutumia maneno yasiyozidi 150, andika habari kuhusu siku ya kwanza ulipoanza Kidato cha Kwanza, kisha waeleze wenzako.

3. Eleza mambo yanayoweza kuathiri mawasiliano baina ya wazungumzaji.

4. Tunga mazungumzo mafupi kati ya:

  1. Mwanafunzi na mwalimu wake kuhusu changamoto za kimasomo
  2. Mjukuu na babu yake kuhusu maadili ya Kiafrika
  3. Mtu mmoja na mwenzake kuhusu biashara anayoifanya

5. Fanya uchambuzi wa ngonjera uliyoisoma hapo awali na ueleze:

  1. Mada kuu ya ngonjera
  2. Kauli mbiu ya ngonjera
  3. Maudhui yaliyojitokeza
  4. Ujumbe wa ngonjera kwa jamii

Mbinu za Kuimarisha Stadi ya Mazungumzo

Njia za Kuboresha Uwezo wa Kuzungumza

1> Mazoezi ya Marudio

Zungumza kwa Kiswahili kila wakati uwezapo, hata kama unazungumza nawe peke yako.

2. Kusikiliza Kwa Makini

Sikiliza vizuri wazungumzaji wengine wa Kiswahili na ujifunze matumizi yao ya lugha.

3. Kusoma Kwa Sauti

Soma vifungu vya Kiswahili kwa sauti ili kujizoeza na matamshi na mtiririko wa maneno.

4. Kujirekodi

Rekodi mazungumzo yako na kuyasikiliza ili kubaini makosa na mambo unayohitaji kuboresha.

5. Kushiriki Katika Majadiliano

Shiriki aktivu katika mijadala na majadiliano mbalimbali ili kujenga ujasiri wako.

6. Kupanua Msamiati

Jifunze maneno mapya kila siku na utumie fursa ya kuyatumia katika mazungumzo yako.

Umuhimu wa Kuzungumza Kwa Ufasaha

  • Hukuza uwezo wa kujieleza kwa uwazi na usahihi
  • Huimarisha uhusiano bora na wengine katika jamii
  • Husaidia katika kufanikiwa katika taaluma na kazi mbalimbali
  • Hukuza kujiamini na kujithamini
  • Husaidia katika kutatua migogoro kwa njia ya amani
  • Hukuza uwezo wa kuwashawishi na kuwaongoza wengine
  • Husaidia katika kuhifadhi na kueneza utamaduni wetu
Sura ya Saba: Kuwasiliana kwa njia ya maandishi

Sura ya Saba: Kuwasiliana kwa njia ya maandishi

Utangulizi

Taarifa au habari iliyokusudiwa huweza kuwasilishwa kwa ufanisi katika muktadha husika kwa njia ya maandishi. Katika sura hii, utajifunza kuwasiliana kwa njia ya maandishi katika miktadha mbalimbali. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kueleza mawazo na taarifa mbalimbali kwa njia ya maandishi katika miktadha mbalimbali. Vilevile, utaweza kuandika matini mbalimbali kwa ufasaha.

Fikiri: Namna unavyoweza kuwasilisha mawazo na taarifa kwa maandishi

Kujieleza kwa maandishi katika miktadha mbalimbali

Soma barua ifuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata:

Shule ya Sekondari Lungo,
S.L.P. 83,
Ngara.
20-03-2020.

Mama mpendwa,

Shikamoo! Habari za hapo nyumbani? Je, baba alifika salama alipotoka huku?

Kusudi la barua hii ni kutaka kukujulisha kuwa nimekwishaanza kuzoea maisha ya hapa shuleni. Tayari tumeanza masomo; kwa hiyo, ninakazana kujifunza na kusoma kwa bidii ili niweze kupata elimu itakayonisaidia kukabiliana na maisha ya kila siku.

Ratiba yetu ya shule huwa inaanza mapema sana. Tunaamka alfajiri na kuchelewa kulala kwa ajili ya kujisomea. Kwa kawaida, tunalala saa me usiku na kuamka saa kumi na moja alfajiri. Vilevile, mchana tunakuwa na kazi za nje. Kazi hizo ni kuchota maji ya kupikia na kuoga. Halikadhalika, tuna muda kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo ili kuboresha afya zetu.

Mama, ninakuomba umkumbushe baba aninunulie vitabu vya Hisabati na Kiswahili.

Ninaishia hapa kwa leo.

Mwanao mpendwa,
Mnyandagaro.

Maswali:

  1. Kuna umuhimu gani wa kujua anwani ya mwandishi wa barua?
  2. Kwa kutumia barua uliyoisoma, barua ya kirafiki ina muundo gani?
  3. Barua uliyoisoma inahusu nini?
  4. Una maoni gani kuhusu ratiba ya shule iliyoelezwa kwenye barua?
  5. Unapaswa kumwandikia barua rafiki yako kumtaarifu kuwa utaenda kumtembelea wakati wa likizo. Andika hatua utakazozingatia katika uandishi wa barua hiyo.

Zingatia

Mawasiliano ya aina yoyote ile hutegemea muktadha unaohusika. Katika kuwasiliana kwa njia ya maandishi unaweza kutumia matini mbalimbali kama vile:

  • Barua
  • Kifungu cha habari
  • Hotuba
  • Risala
  • Kumbukumbu za mikutano
  • Insha

Kuna mambo kadhaa ambayo mwandishi anapaswa kuzingatia ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa:

  • Mwandishi anapaswa kuzingatia ufasaha wa lugha anayoitumia ili msomaji aweze kuelewa ujumbe uliokusudiwa.
  • Aidha, anapaswa kuzingatia matumizi ya lugha fasaha kwani yatamsaidia msomaji kuelewa na kukuza lugha inayohusika kwa ufasaha.
  • Vilevile, mwandishi anapaswa kutumia msamiati sahihi unaoendana na muktadha wa mada inayohusika.
  • Halikadhalika, anapaswa kuzingatia uhusiano sahihi wa maneno ili kujenga sentensi zinazoeleweka kwa msomaji.
  • Pia, matumizi sahihi ya viunganishi na tahajia yanapaswa kuzingatiwa.

Pamoja na hayo, katika kukuza stadi ya kuandika, ni muhimu kuzifahamu vyema alama za uandishi ili maudhui yaliyokusudiwa yaweze kumfikia msomaji. Alama hizo ni kama vile:

  • Alama ya kuuliza (?)
  • Nukta (.)
  • Mkato (,)
  • Funga na fungua semi (" ")
  • Nukta pacha (:)
  • Nukta mkato (;)
  • Kistari (-)
  • Mstari wa mshazari (/)
  • Mabano (( ))
  • Alama ya mshangao (!)
  • Nukta katishi (…)
  • Ritifaa (’)

Aidha, matumizi ya herufi kubwa yanapaswa kuzingatiwa. Alama hizi huwa na dhima mbalimbali katika matini inayoandikwa ikiwa ni pamoja na kuonesha mipaka ya sentensi na vituo.

Zoezi la 7.1

Andika barua rasmi kwa msimamizi wa maktaba ya shule yako ukiomba kuazima vitabu vinavyohusu uandishi wa insha na barua rasmi.

Zoezi la 7.2

Sikiliza hotuba mojawapo ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutoka vyanzo mbalimbali kisha andika muhtasari wa hotuba hiyo kwa maneno yasiyozidi 100.

Shughuli ya 7.2

Fikiri kwamba wewe ni kiongozi wa wanafunzi na umehudhuria mkutano wa kufungua shule na unapaswa kuandika kumbukumbu za kikao ulichokihudhuria; andika kumbukumbu za mkutano huo.

Zingatia

Kuna utaratibu maalumu ambao huzingatiwa katika uandishi wa aina yoyote ile:

  1. Kwanza, telewe vyema jambo unaloliandikia. Hii itakusaidia kuliandika kwa upana na kufikisha ujumbe kamili kwa hadhira inayohusika.
  2. Pili, kumbuka kufuata mtiririko mzuri wa mawazo ili kupangilia maudhui vizuri na kufanya yaeleweke kwa msomaji.
  3. Tatu, ni muhimu kutumia lugha fasaha.

Haya yote yatakuwezesha kufikisha ulichokikusudia kwa uwazi na utamwezesha msomaji kupata uelewa wa jambo uliloliandika na ujumbe uliokusudiwa.

Shughuli ya 7.3

1.(a) Tafuta matini inayohusu haki za binadamu kutoka katika vyanzo mbalimbali vikiwemo vyanzo vya nkondoni.

(b) Andika ripoti fupi kuhusu matini uliyoisoma kwa kuzingatia yafuatayo:

  • (i) Mwandishi wa matini hiyo
  • (ii) Mambo yanayozungumziwa katika matini uliyoisoma
  • (iii) Funzo ulilolipata kutokana na matini uliyoisoma

Zoezi la marudio la 7

1. Oanisha maana zilizopo katika Orodha A na dhana zilizopo katika Orodha B kwa kuandika herufi ya jibu sahihi.

Orodha A Orodha B
(i) Hutumika kuonesha maelezo ya ziada au ufafanuzi wa maneno A. mkato
(ii) Hutumika kuuliza swali B. nukta
(iii) Hutumika kuonesha mwisho wa sentensi C. alama ya mshangao
(iv) Hutumika kuonesha hisia za mzungumzaji D. nuktamkato
(v) Hutumika kuonesha maneno halisi ya mzungumzaji E. kiulizo
F. alama za mtajo
G. mabano

2. Fafanua mambo ya kuzingatia katika uandishi bora.

3. Fikiri kwamba unapaswa kuandika barua kwa wazazi wako kuwataarifu kuhusu kufunga shule na kuomba wakutumie hela ya nauli. Eleza kwa ufupi mambo utakayoyazingatia katika barua yako, kisha iandike.

4. Soma kifungu cha habari kifuatacho, kisha kiandike kwa kufuata taratibu za uandishi. Andika kichwa cha habari, tenga aya, na utumie alama za uandishi na herufi kubwa kwa usahihi.

kubo ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza anayependa sana kujisomea hujisomea masomo yote ili aweze kupata maarifa ujuzi na umahiri wakati wa vipindi darasani hutulia kumsikiliza mwalimu mwalimu asipokuwepo hutumia muda huo kujisomea Siku moja wakati wa somo la Kiswahili alichaguliwa kusoma insha alisoma vizuri sana sisi sote pia tulisoma vizuri kwa sababu tunapenda kusoma pia mwalimu alituambia jipongezeni tukajipongeza kwa makofi paa paa paa ilipofika wakati wa somo la kingereza kubo alijibu maswali mengi kuliko sisi mwalimu alimpongeza sana kubo alisema kuwa wote tuige mfano wa kubo kwa sababu ni muhimu kuelewa vizuri kila somo tangu siku hiyo wanafunzi wote tulianza kujisomea darasani kama kubo ili tuweze kufanya vizuri katika masomo yote tuling'amua kwamba hii statusaidia kupata elimu itakayotuwezesha kukabiliana na mazingira ya kila siku

No comments

Post a Comment

© all rights reserved
made with by templateszoo